×

Hawa Ndiyo Wakongwe Waliofanya Albam Nyingi Zaidi Bongo

MIAKA ya nyuma mafanikio ya msanii ilikuwa ni kuwa na album ambayo ilikuwa kama utambulisho wa msanii katika kazi zake. Album zilikuwa zikifanya poa kiasi kwamba, kuwafanya wasanii kutoa sana album kuliko single (ngoma mojamoja).

 

Japo kwa sasa soko la album limeshuka, lakini wapo wasanii ambao wanatoa albam kama tulivyoona kwa, Diamond Platnumz, King Kiba, Rayvanny, Harmonize na wengine wengi.

Leo tutajikumbusha wasanii wa Bongo ambao huko nyuma walitoa albam kwa wingi na wakaheshimika katika soko la muziki Bongo.

 

MR 2/SUGU

Jina halisi ni Joseph Mbilinyi almaarufu Mr 2 au Sugu. Ni miongoni mwa waanzilishi wa awali wa Hip Hop Bongo. Sugu alitamba na ngoma yake ya Wananiita Sugu. Ni msanii wa kwanza mwenye album kumi katika soko la muziki Bongo, album kama Ni Mimi ya mwaka 1995, Ndani ya Bongo (1996), Niite Mr 2 ya (1998), Nje ya Bongo (1999), Millenia (2000), Muziki na Maisha (2001), Itikadi (2002), Sugu (2004), Coming of Age (2006), VETO (2009) na Anti-Virus Mixtapes. Sugu kwa sasa ni mwanasiasa na aliwahi kuwa Mbunge wa Mbeya- Mjini kwa tiketi ya Chadema.

 

PROF JAY

Joseph Haule au Profesa Jay ni msanii ambaye yupo kwenye kiwanda cha Hip Hop Bongo. Alifanikiwa kuwateka mpaka wazee kusikiliza muziki wake akiwemo Jaji Joseph Sinde Warioba. Alitamba sana na ngoma ya Zubeda ambayo ilifanya poa kwa miaka mingi.

 

Album zake ni sita; Machozi, Jasho na Damu ya mwaka 2001, Mapinduzi Halisi (2003), Joseph (2006), Aluta Continua (2007), Izack Mangesho (2014) na Kazi Kazi (2016). Profesa Jay bado anafanya poa katika muziki na alijikita zaidi kwenye siasa, kwani alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi mkoani Morogoro kupitia Chadema.

 

LADY JAYDEE

Malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura au Lady Jaydee au Jide ametamba na ngoma ya Machozi. Amebeba heshima katika medani ya muziki kuanzia mwaka wa 2000 mpaka akaitwa Komando baada ya kutoa albam yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Machozi na kutoa single kadhaa kutoka kwenye albam hiyo na kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza katika Bongo Fleva kutumia gharama kubwa ya kuandaa album.

 

Album nyingine alizotoa ni kama Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jay Dee (2012), Nothing But The Truth (2013), Woman (2017), 20 (2021) na kadhalika.

Mbali na ukongwe kwenye gemu, bado Lady Jaydee anafanya poa kwani alishiriki katika ngoma mpya ya Harmonize inayokwenda kwa jina la Wife na ikafanya vizuri sana kwenye mtandao wa YouTube.

MAKALA: ELVAN STAMBULI

Leave a Comment