
MAMA anayetuhumiwa kuwaua wanawe wawili na kujeruhi watatu kwa sumu ya kuua wadudu kwenye nyanya, imebainika ametelekezwa na wanaume watano aliozaa nao kila mmoja mtoto mmoja.
Mama huyo, Veronica Gabriel (30) hivi sasa ana ujauzito wa miezi mitatu na wanawe wamelazwa kituo cha afya Bwanga wakiendelea na matibabu.
Akisimulia mkasa wake mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule kumtembelea, alisema aliamua kuwapa watoto wake sumu na yeye mwenyewe kunywa baada ya kutengwa na ndugu na wanaume wanaomzalisha.
Tukio la mama kuwapa sumu watoto na yeye mwenyewe kunywa kwa lengo la kujiua kutokana na ugumu wa maisha, lilitokea Desemba 1, majira ya saa 11 jioni huko Buseresere wilayani Chato mkoani Geita.
Alisema amekuwa akiishi maisha magumu bila msaada, hivyo kuona bora kujiua ili mateso yaishe na wanaume waliomzalisha hukutana nao kwa lengo la kumsaidia mlo wa siku na watoto wake, mwisho wa siku hujikuta amepata ujauzito na mwanamume kumtelekeza.
“Siwatambui wanaume niliozaa nao maana huwa nakutana nao kimwili siku moja na najikuta nina mimba, huwa nawakuta njiani hata kwao sipajui, wakati mwingine hata jina siwafahamu ila nikikutana nao njiani nawafahamu sura,” alisema Veronica.
Aomba kifungo bila mateso
Veronica alisema anatambua ametenda kosa na yupo tayari kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, lakini anaomba Serikali kumhurumia na endapo atafungwa anaomba asiteswe kwa kuwa ameshateseka na maisha ya dunia.
Kwa upande wa Senyamule, alisema maisha magumu ndiyo yamemfanya mama huyo kukata tamaa ya maisha na kuitaka idara ya ustawi wa jamii kufuatilia watoto watatu waliobaki na kuona ni namna gani watapata haki ya kuishi, kutunzwa na kuanzishwa shule.
“Waje watuambie watoto hawa wataishi vipi, awali walikuwa wanaishi na mama yao ambaye yupo chini ya vyombo vya usalama, pia tusifanye ngono isiyo salama, inasababisha mtu kupata mtoto asiyetarajiwa,” alisema Senyamule.
Naye Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Bwanga, Magreth Kimwaga alisema mama na wanawe wanaendelea vizuri na uchunguzi waliofanya kwenye miili ya watoto wawili imebainika vifo hivyo vimetokana na athari ya sumu waliyopewa.
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Henry Mwaibambe alisema watamhoji mama huyo ili kuwapata wanaume waliompa mimba na sheria ichukue mkondo wake kwa kosa la kutelekeza watoto.