
JESHI la Polisi mkoani Geita limejipanga kuwatumia maofisa wa jeshi hilo zaidi ya 754 waliotoka mafunzoni ili kusaidia kudhibiti matukio ya ajali za barabarani na kuimarisha usalama mwishoni wa mwaka huu.
Hatua hiyo ya Mkoa wa Geita imeelezwa pia kufanyika katika mikoa mingine ingawa hawakuwa tayari kutaja idadi ya askari watakaopelekwa barabarani.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa alisema ni kawaida katika sikukuu za mwishoni mwa mwaka kikosi chake kushirikiana na askari polisi wengine katika kusimamia usalama barabarani.
Mutafungwa alisema kila mkoa unakuwa na utaratibu wake wa namna ya kuwapanga askari hao katika kusaidia kusimamia usalama barabarani.
Katika taarifa yake kuhusu Geita, Kamanda Polisi mkoani hapa, Henry Mwaibambe alisema mkoa huo kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka umejipanga kuhakikisha hakuna ajali.
Mwaibambe alisema kihistoria msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya umekuwa ukiambatana na ongezeko la ajali hivyo maofisa hao watasambazwa maeneo yote mkoani hapa kusimamia sheria.
“Dereva yeyote yule ambaye atashindwa kufuata sheria za usalama barabarani hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake, lakini kwa wananchi nao wafuate sheria za barabarani, siyo magari tu,” alisema.
Aidha, Kamanda Mwaibambe amepiga marufuku wananchi kulipua fataki bila kibali maalumu kwa kuwa huenda ikasababisha tishio la usalama na vitendo vya uhalifu kwa watu wasio waaminifu.
Aliongeza kuwa: “Pia ni marufuku kupiga honi ovyo mitaani na barabarani… tunasema kupiga honi ovyo ovyo hairuhusiwi.
“Siyo kupiga honi ila ni kupiga honi ovyo, ambayo inaweza kusababisha kero kwa watu wengine, hata kama ni harusi ni lazima kuwe na utaratibu, lazima sheria zifuatwe na kibali kizingatiwe.”
Mwaibambe aliwataka wananchi wanaosafirisha mizigo kwa kutumia wanyama kazi ikiwemo punda na ng’ombe kutofanya hivyo nyakati za usiku kwani imekuwa chanzo cha ajali.
“Mwisho wa mwaka kuna matukio mengi sana ya uhalifu, wengine wanasema eti wanatafuta pesa ya sikukuu, tumejipanga kwa hilo, tumeimarisha doria,” alisisitiza Mwaibambe.