NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha maboresho yanayofanywa katika ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yanakamilika ifikapo Juni mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi huo, Kasekenya amewataka wataalam wanaosimamia maboresho ya barabara hiyo waendelee na zoezi la utoaji elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara hiyo ili kupunguza ajali.

“…TANROADS shirikianeni na askari wa usalama barabarani kutoa elimu ya namna bora ya kutumia vivuko vya juu na chini ya barabara pindi ujenzi wake unapokamilika na kuhakikisha barabara zinakuwa safi wakati wote,” amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Amewaonya wote wanaoharibu alama za barabara na kutupa taka ngumu kuacha mara moja uharibifu huo na kuwataka wasimamizi wa barabara kuwachukulia hatua za kisheria mara moja.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Harun Senkuku amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yenye urefu wa KM 19.2, uliohusisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji umekamilika na kinachoendelea sasa ni uboreshaji wa njia ya mwendokasi katika barabara hiyo.