×

Msemaji wa Serikali Anusurika Katika Shambulio la Bomu

Waziri Mkuu wa Somalia, Mohamed Hussein Roble amesema msemaji wa serikali ya nchi hiyo, Mohamed Ibrahim Moalimuu amejeruhiwa katika shambulio baya la kigaidi kwenye gari lake jana Jumapili, Januari 16, 2022 ambapo hali yake inaendelea vizuri.

 

Moalimuu, alipelekwa hospitalini baada ya mlipuko wa bomu kwenye makutano ya barabara katika mji mkuu, Mogadishu ambapo Kundi la wanamgambo wa kiislamu la al-Shabab limedai kuhusika na tukio hilo.

 

Moalimuu ambaye ni mwandishi wa habari wa zamani wa BBC amenusurika katika mashambulizi kadhaa ya hapo awali kabla ya hili lililotokea jana.

 

Shambulio hili la hivi karibuni la bomu katika mji mkuu linakuja siku chache baada ya lingine lililoua takriban watu wanane – lile lililotekelezwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab karibu na kambi ya Jeshi la Wana-anga la Somalia na uwanja wa ndege wa kimataifa.

 

Al-Shabab imekuwa ikipambana na serikali ya Somalia kwa zaidi ya muongo mmoja, na inashikilia ngome katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

 

Mashambulio haya ya hivi karibuni yanatokea huku kukiwa na mvutano wa kisiasa wa miezi kadhaa kati ya waziri mkuu na rais kuhusu uendeshaji wa uchaguzi uliocheleweshwa.

 

“Inaonekana hali imetulia kwa sasa,” mwandishi wa habari wa Somalia Mohamed Mohamed aliiambia BBC Focus on Africa radio mapema wiki hii.

 

“Viongozi wa kanda na waziri mkuu wameweza kupata makubaliano ambayo yanaharakisha uchaguzi ndani ya siku 40 – kuanzia tarehe 15 Januari.”

Mapema mwezi huu, takriban watu wanane waliuawa katika mlipuko wa bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, waokoaji wamesema. Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab limesema lilitekeleza shambulio hilo.

 

Mlipuko huo ulitokea kwenye barabara ya eneo la kuingia kambi ya Jeshi la wana anga la Somalia ambalo iko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa.

 

Walioshuhudia tukio hilo wameliambia shirika la habari la AFP kwamba msafara wa usalama wa kibinafsi, ukiwasindikiza wageni, ulikuwa ukipita wakati bomu hilo likilipuka.

 

“Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba umeharibu majengo mengi yaliyo karibu na barabara na magari yanayopita eneo hilo,” Hassan Nur alisema.

 

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ya kujitoa mhanga. Somalia pia iko katikati ya mzozo wa kisiasa kutokana na mzozo wa madaraka kati ya rais na waziri mkuu kabla ya uchaguzi.

Leave a Comment