
Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Uledi Abbas Mussa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kipindi cha miaka mitatu.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu inaeleza kuwa uteuzi huo umeanza Desemba 23, 2021 ambapo Mussa anachukua nafasi ya Dkt. Suleiman Magesa Misango ambaye anaendelea na majukumu yake ya ukurugenzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mussa ni Katibu Mkuu Mstaafu na Mshauri Binafsi wa Masuala ya Kiuchumi wa Kimataifa wa GFA Consulting Group, tawi la Tanzania.
Mnamo Machi 15, 2017, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitengua uteuzi na kumsimamisha kazi Uledi ambaye kwa kipindi hicho alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 15, 2017 na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Eng. John Kijazi, hatua hiyo ilichukuliwa ili kupisha uchunguzi zaidi dhidi ya Uledi kufuatia kutozingatiwa kwa taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia masuala ya uwekezaji.