
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amemteua msanii wa muziki, Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ kuwa Balozi wa Sekta ya Maji nchini ambapo atakuwa akiitangaza Sekta ya Maji kupitia kazi yake ya sanaa anayoifanya katika shughuli mbalimbali za Kiserikali na zisizo za Kiserikali.
Uteuzi huo umekuja baada ya Mjomba huyo kuimba wimbo wenye maudhui bora na kusheheni takwimu sahihi kuhusu miradi mbalimbali ya maji inayoendelea kujengwa nchini na ile iliyokamilika, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Bunda Mkoani Mara, ambayo ilihudhuriwa na Rais Samia.
Wakati akihutubia leo mara baada ya kusikia ujumbe wa Mrisho Mpoto aliyetumbuiza pamoja na msanii mwenzake, Peter Msechu, Rais Samia alimuomba Waziri wa Maji amfanyie jambo Mrisho Mpoto, na jambo lenyewe ndio hilo shavu la ubalozi ambalo Mjomba amelipata.
Hii si mara ya kwanza kwa Mjomba kupata dili kama hili, ikumbukwe pia kuwa Mrisho Mpoto ni balozi wa Sekta ya Utalii nchini, pia ni balozi wa mazingira kupitia kampeni ya Nyumba ni Choo na endorsement nyingine nyingi ambazo amekuwa akizipata kupitia Serikali na watu binafsi.
