×

Waasi ADF Wanaodaiwa Kuwa ni Watanzania Wakamatwa DRC

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vimetangaza kuwakamata raia watatu wa Tanzania wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa kundi la waasi la ADF waliosajiliwa Beni, Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza, BBC raia hao wa Tanzania, walikamatwa Jumapili ya Februari 6, 2022 wakati wa doria zilizofanywa na askari wa DRC katika Bonde la Mwalika, Wilaya ya Beni Jimbo la Kivu Kaskazini.

BBC imemnukuu msemaji wa Tarafa ya Sokola 1, Kivu Kaskazini, Kapteni Athony Mwalushayi akieleza kuwa waasi hao wamekiri kuwa walisajiliwa kwa nia mbaya na raia mmoja wa Kongo ambaye aliwarubuni kwamba watafanya kazi katika migodi ya dhahabu, lakini wakajikuta katika kundi hilo la waasi.

Akizungumza na BBC, Kapteni Mwalushayi amesema waasi hao wamekabidhiwa kwenye mikono ya idara husika ili waandelee kuchunguzwa.

Januari 28, mwaka huu katika eneo hilohilo la Beni, FARDC pia lilimkamata muasi wa ADF, raia wa Kenya, Salim Muhammad, ambaye alikuwa anasambaza video za ukatili.

Leave a Comment