
SERIKALI kupitia idara ya Habari Maelezo imesema itaunda kamati maalum ya wanahabari na wadau wa habari nchini kujadili na kupitia upya sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau kwa muda mrefu kuwa ni kandamizi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza kwenye mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari nchini Alhamisi, Februari 10, 2022 jijini Dar es Salaam.
Nape amesema sheria hiyo ina mapungufu mengi na mambo yamebadilika tangu ilipotungwa mwaka 2016 mpaka sasa 2022 na kuiagiza Idara ya Habari Maelezo kuunda kamati hiyo mapema.
“Mwenyekiti wa TEF alikuwa ananisumbua tukutane, nikamwambia siwezi kuja mikono mitupu, tunashukuru kwa kuitikia wito huu wa kuja. Mmetupa heshima ya kuja kuzungumza na sisi, niliwamisi sana.
“Mimi nikiwa Waziri nakumbuka nilisimamia sheria ile (sheria ya habari), wakati ni tofauti na sasa, haiwezi kufanana!, kwahiyo tutaipitia tutakubaliana yatakayowezekana tutayabadilisha kwa sababu ni maagizo ya Rais, sisi kazi yetu ni kutekeleza.
“Mimi ni mwanahabari mwenzenu tuaminiane,nia njema lakini ukikutana na jiwe!? Usigeuke ila rudi nyuma kidogo halafu nenda pembeni endelea na safari,Jiwe litashughulika na Mwenyezi Mungu baadae kwasababu inawezekana likayeyuka,likazama au likafanyaje.
“Tutaunda kamati ndogo itakayohusisha wanahabari, tufanye mashauriano na Serikali tupitie kifungu kimoja hata kingine tuone ni namna gani wapi tunakubaliana tupeleke Bungeni tuone namna ya kuipitia upya sheria ya habari hapa Nchini.
“Nimezielekeza taasisi zilizokuwa zinasita kutoa matangazo na kulipa madeni, zitoe matangazo na madeni. Hatuna sababu ya kubaguana, wote mna macho sawa. Niwaombe wanahabari tuaminiane, mimi mwandishi wa habari mwenzenu. Hiki ninachokieleza ndicho kipo kwenye moyo wa Rais Samia na uelekeo wa serikali ya awamu ya sita, tufanye kazi pamoja.
“Tutatumia busara, tutashikamana kwa pamoja na nia ya Serikali ya awamu ya sita ni nzuri. Mimi najua tulikotoka, wakati mwingine safari ya mabadiliko ni ndefu. Tunaomba tuaminiane tutafika. Serikali ya awamu ya sita inataka kuboresha mahusiano yaliyopo kati ya wanahabari, vyombo vya habari na sekta binafsi. Kwa hiyo toeni maoni na ushauri sisi tutayafanyia kazi,” amesema Nape Nnauye.