
RAIS wa Urusi Vladimir Putin amelitaka jeshi la Ukraine kuiondoa madarakani serikali ya rais Volodymyr Zelensky Akilihutubia baraza la usalama la nchi hiyo kuhusu mwenendo wa uvamizi wa taifa hilo kwa Ukraine, Putin ameseme “Nawaeleza wanajeshi wa Ukraine kwa mara nyingine tena: usiruhusu Neo-Nazis na Banderites kutumia watoto wenu, wake zenu na wazee kama ngao zao.
“Chukueni mamlaka mikononi mwenu mwenyewe. Inaonekana kama nyie na sisi tunaweza kupata suluhu kirahisi kuliko genge hilo la waraibu wa madawa ya kulevya na Neo-Nazis huko Kyiv.
Mara kadhaa Putin amekuwa akilitumia neno la Neo-Nazis kuirejea Serikali ya Ukraine, na Bandera akifananisha na mpinga Muungano wa Sovieti maarufu aliyepigana kwenye vita vya pili vya dunia, Stepan Bandera.
Rais wa Ukraine Zelensky ambaye ni myahudi, amekuwa akipinga serikali yake kupewa majina ya aina hiyo na sifa za genge la dawa za kulevya.
Rais Putin anazungumza sasa, huku vikosi vya taifa hilo vilivyoivamia Ukraine vikizidi kusonga mbele kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake vimechukua udhibiti wa uwanja muhimu wa ndege wa Hostomel karibu na Kyiv. Inadai pia wanajeshi 200 kutoka vitengo maalum vya Ukraine waliuawa na hakukuwa na majeruhi wa Urusi. Ukraine wao wanadai askari 1,000 wa Urusi wameuawa tangu uvamizi huo wa wiki hii, kama ilivyo kwa madai mengine kuhusu takwimu za mauaji, hatuwezi kuthibitisha hili.
Umoja wa mataifa umesema zaidi ya watu 100,000 wameikimbia Ukraine kwa ajili ya usalama wao, huku wengine milioni 5 walikatajiwa kuikimbia nchi hiyo.
Pande zote mbili za mzozo huo, zimeonyesha ziko tayari kwa mazungumzo, kwa masharti yasiyotatiza maslahi yao.