×

Taleban Yawazuia Wananchi Kusafiri Afghanistan

Serikali ya Taleban inayoongoza nchini Afghanistan, imewapiga marufuku wananchi wa nchi hiyo kusafiri kwenda nje ya nchi bila kuwa na sababu maalum.

 

Marufuku hiyo imetangazwa na Msemaji wa Taleban, Zabihullah Mujahid na kueleza kuwa hatua hiyo ina lengo la kuzuia wananchi wa Afghanistan kwenda kupata taabu nje ya nchi hiyo.

 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa safari za kuwaondoa nchini humo wananchi mbalimbali kwenda kupatiwa hifadhi katika mataifa mengine zilizokuwa zinafanywa na mataifa mbalimbali na mashirika yasiyo ya kiserikali, pia zimesitishwa.

 

Mujahid ameeleza kuwa hata wanawake ambao watakuwa na sababu maalum za kusafiri kwenda nje ya nchi hiyo au kutoka mji mmoja kwenda mwingine, wanapaswa kusindikizwa na ndugu wa kiume kama ilivyotangazwa tangu mwaka jana.

 

Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya serikali ya Taleban, kuanza oparesheni maalum ya kuwasaka nyumba kwa nyumba watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu wakiwemo watekaji nyara, wezi na vibaka.

 

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu, yamelaumu hatua hiyo na kueleza kwamba inawanyima haki ya msingi raia wa Afghanistan waliokuwa na mipango ya kwenda kutafuta hifadhi katika nchi nyingine, kufuatia hali tete ya usalama tangu kundi hilo lilipochukua madaraka.

Leave a Comment