×

Vita Ukrain Yaiweka Afrika Mtegoni

Vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine inayaweka mataifa ya Afrika katika msemo wa kimakonde ‘ukisimama nchale, ukikimbia nchale’.

 

Salama ya kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa na kijeshi kwa Afrika inapita kikaangoni hasa linapokuja suala la upande upi wa kuunga mkono, kati ya Ukraine na Urusi.

 

Urusi ambayo ni taifa lenye nguvu kiuchumi na kijeshi duniani, inadaiwa kusapotiwa na washirika wake, China na Korea Kaskazini huku Ukraine ikikumbatiwa na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi ‘NATO’ na Marekani.

NATO inayoundwa na mataifa makubwa ya Ulaya kama Uingereza na Ujerumani imejiingiza vitani kwa mlango wa nyuma kwa kuisaidia silaha Ukraine, huku Umoja wa Ulaya ukiidhoofisha Urusi kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

 

Sauti za kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine zinasikika zaidi kutoka upande wa washirika wa NATO na Marekani, huku upande wa pili ukionekana kujizua kusema lolote na kutaka suluhu ipatikane.

 

Swali linakuja, Afrika isimame wapi katika vita hivi hasa ukizingatiwa kwamba mataifa yake ni ‘tegemezi’ kwa pande zote zinazozozana?

Ni kama kusema “Baba kaniita na mama kaniita niende kwa nani; wote ni wangu?” Afrika ikichagua Urusi, mataifa ya Ulaya yatanuna na ikichagua Ukraine; Urusi na washirika wake nao watanuna sana.

 

Kibaya kilicho wazi ni kwamba, hakuna upande unaoonekana dhaifu; ungekuwepo ingekuwa rahisi kwa mataifa ya Afrika kufungamana na upande wenye nguvu kufanya mambo yasiwe mengi, maana kumsaidia asiye na nguvu “mtapigwa wote.”

 

Afrika ichague nini kwenye vita hii hasa linapokuja suala la utekelezwaji wa vikwazo alivyowekewa Urusi na uungaji mkono kijeshi; itafune au imeze?

 

Nionavyo; BORA KUKAA KIMYA kwa sababu Afrika ilishapita kwenye upepo wa siasa zisizofungamana na upande wowote.

Hata kwenye hii vita bora isifungamane na upande wowote; iwaache wenyewe wapambane.

 

STORI NA RICHARD MANYOTA

Leave a Comment