
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Belarus ambaye pia ni mwanajeshi mwenye cheo cha Meja Jenerali, Viktor Gulevich ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake na kueleza kwamba hayupo tayari kuunga mkono uamuzi wa Belarus kuisaidia Urusi katika uvamizi unaoendelea nchini Ukraine.
Kiongozi huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi waliotangazwa kuwekewa vikwazo na Uingereza na rafiki wa karibu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi, ndiye awali aliyeidhinisha uamuzi wa majeshi ya Belarus kuingia nchini Ukraine kwenda kuungana na majeshi ya Urusi.
Amedai kuwa sababu kubwa ya kuchukua uamuzi huo, ni kutokana na kukataliwa kwa mawazo yake na viongozi waliopo chini yake na kuleta mgawanyiko katika vikosi vilivyoingia nchini Ukraine, wengi wakionesha kutounga mkono uvamizi wa Urusi nchini humo.
Gulevich ambaye pia ndiye mshauri mkuu wa rais wa masuala ya usalama nchini Belarus, amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa waziri wa ulinzi akieleza kuwa viongozi wa kijeshi waliopo chini yake, wamekataa kutii maagizo ya kuungana na Urusi kuishambulia Ukraine.