
Vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi yake kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev, wakati ambapo wapatanishi wanakutana tena katika duru nyingine ya mazungumzo ya kusitisha mapigano.
Mashambulizi hayo yaliyofanyika mapema Jumanne asubuhi kwenye maeneo ya makaazi ya watu mjini Kiev, yamewaua takribani watu wawili.

Jengo la ghorofa 16 katika wilaya ya Sviatoshynsky na jingine lenye ghorofa 10 kwenye eneo la Podilsk yameshambuliwa katika mashambulizi hayo ya anga. Maafisa wa huduma za dharura wamesema kuwa zaidi ya watu 27 wameokolewa katika mashambulizi hayo.
Urusi yaudhibiti mkoa wa Kherson
Huku hayo yakijiri, jeshi la Urusi limesema limechukua udhibiti kamili wa mkoa wa Kherson kusini mwa Ukraine. Eneo hilo lililoko katika Bahari Nyeusi ni makaazi ya watu wapatao milioni moja. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema pia majeshi ya Urusi yamedhibiti maeneo mingine.

”Vikosi vya wanajeshi vya shirikisho la Urusi vimechukua udhibiti kamili wa eneo lote la mkoa wa Kherson. Wakati vikosi vyetu vinaendelea na mashambulizi, vimeliteka pia eneo la makaazi la Stepne. Kundi la wanajeshi wa Jamhuri ya watu wa Luhansk linaendesha operesheni katika wilaya za kaskazini mashariki mwa mji wa Severodonetsk,” alifafanua Konashenkov.