×

Steve Nyerere: Sitoki Ng’o, Mniombe Radhi – Video

MUIGIZAJI Steve Nyerere, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa msemaji wa shirikisho la muziki nchini, leo Machi 22, 2022, amezungumza na wanahabari kuhusiana na yanayoendelea baada ya wasanii wengine kuibuka na kumpinga.

 

KAMA ulitarajia msanii Steve Mengele a.k.a Steve Nyerere, ataachia nafasi ya usemaji wa Shirikisho la Muziki nchini (Shimuta), kutokana na kupingwa na baadhi ya wasanii, utakuwa umekosea sana.

 

Ndiyo utakuwa umekosea, kwani msanii huyo amesema hana ndoto za kuachia nafasi hiyo, badala yake ndo ameimarika zaidi kuhakikisha anawasemea wanamuziki nchini na kuwapa saa 48 waliokuwa wanampinga kumuomba radhi na pia kuwaomba radhi wanamuziki wengine.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22, 2022 jijini Dar es Salaam, Steve amesema hata kikao kilichofanyika jana kwa baadhi ya wasanii kumshambulia kilikuwa batili.

 

“Nazungumza hapa nikiwa msemaji wa Shirikisho la Muziki Tanzania (Shimuta), hivyo nasema kazi iendelee.

“Waliowadharau viongozi wa Shimuta waombe radhi, kuanzia muziki wa injili, taarabu, dansi na wengine wote.

“Yameitwa majina ya ajabu sana, hata wasanii wa vichekesho wamedharauliwa, kuna haja ya kuombwa radhi, wamezungumzia hadi mambo ya elimu, nafikiri sio sahihi.

 

“Walitakiwa kunikaribisha na kunisikiliza, nina sera zipi, sio kunilaumu bila sababu ya msingi. Walitakiwa kuniambia changamoto zao kuwa hawana studio, umoja wao sio mzuri, wamefeli wapi, nini tufanye kupata maendeleo,” amesema Steve Nyerere.

 

Hata hivyo amesema atajitoa katika nafasi hiyo kama viongozi wa juu wa Shimuta wakimtaka aondoke, ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi na Mhazini watamtaka afanye hivyo na wala si vinginevyo.

 

Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Shimuta, Ado Novemba alimtambulisha Steve Nyerere kuwa Msemaji wa shirikisho lao, uamuzi ambao ulizua mjadala kwa baadhi ya wasanii wakipinga uteuzi huo.

 

Jana baadhi ya wasanii walikutana jijini Dar es Salaam, ambapo msanii Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, alisema baada ya kikao hicho kuwa wametoa saa 48 kwa Steve Nyerere kuachia wadhifa huo, kwani wao hawana shida ya kusemewa na yeye.

Leave a Comment