×

Katibu Mkuu Wa Kwanza Mwanamke Marekani Afariki Dunia

MADELEINE Albright ambaye ndiye aliyekuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa katibu mkuu kiongozi wa Marekani, amefariki dunia leo Jumatano, Machi 23, 2022 akiwa na umri wa miaka 84.

Albright ambaye alizaliwa nchini Czechoslovakia, ni miongoni mwa wanawake wa mwanzo kabisa kuaminiwa na kupewa dhamana ya uongozi katika ngazi za juu nchini Marekani ambapo familia yake imesema alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani.

Enzi za uhai wake, mwanamama huyo ambaye kitaaluma alikuwa profesa wa sayansi ya siasa, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo kuwa mshauri wa Bill Clinton kuanzia mwaka 1993 ambapo pia aliteuliwa na Clinton kuwa balozi wa Marekani katika Baraza la Umoja wa Mataifa (UN).

Akiwa katika wadhifa huo, Albright aliweka rekodi ya kufanya ziara nyingi zaidi nje ya Marekani, akizitembelea nchi 98, rekodi ambayo ilikuja kuvunjwa na mwanamama mwingine, Hillary Clinton mwaka 2012 ambaye alizitembelea nchi 102.

Sifa nyingine aliyokuwa nayo mwanamama huyo, ni uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha mkubwa lugha mbalimbali za mataifa, ikiwemo Kiingereza, Kifaransa, Kirusi, Kiserbia, Kipoland na Ki-Czech.

Inaelezwa kwamba enzi za utawala wake, mwanamama huyo alifanya kazi kubwa ya kutengeneza sera za kudumisha usalama mashariki ya kati, kuboresha uhusiano kati ya Marekani na China na Urusi pamoja na kuutanua Umoja wa Kujihami wa NATO kwenye nchi nyingi za Ulaya.

Leave a Comment