
MOTO uliolipuka ghafla Jumatano Aprili 6, 2022 umeteketeza eneo la kuhifadhia mafuta ghafi linalomilikiwa na Mamlaka ya Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba aliyetembelea eneo hilo, Meneja Opereseni wa kampuni ya Mohaza inayotunza mafuta ghafi katika eneo la tukio, Ramadhani Mambya amesema moto huo umesababishwa na kulipuka kwa mota iliyokuwa ikikoroga mafuta hayo kwa ajili ya kupakuliwa.
“Kulikuwa na vijana waliokuwa wakichukua haya mafuta mazito wanayaweka pale chini halafu yanasagwa kisha yanapakiwa kwenye lile tenki. Sasa nafikiri ni ajali tu imetokea, kwa sababu ile mota inayozungusha ndiyo imelipuka ukizingatia kwenye lile kontena ilikuwa na mafuta yaliyolainishwa,” amesema.
Aidha amesema mafuta hayo yalikuwa yanapakiwa na kampuni za Wachina na yalikuwa yakipelekwa nchini Uganda na kwamba hutumika pia kwenye viwanda vya vyuma.