×

Tarura Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Faini za Wakwepa Kodi za Maegesho


Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unapenda kuwataarifu wananchi kuwa
umeanza rasmi kutoza faini kwa watumiaji wa maegesho waliopitisha Siku 14 bila kulipa madeni
ya Ushuru wa Maegesho.

 

Kwa mujibu wa Kanuni ya 9 (3) ya Kanuni za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Usimamizi na Uendeshaji wa Maegesho wa Vyombo vya Usafiri katika Hifadhi za Barabara) Tangazo la Serikali Na. 799 lililochapishwa tarehe 03/12/2021 “Kila mmiliki wa chombo cha usafiri kinachoegeshwa katika maegesho atakuwa na wajibu wa kulipa ushuru wa maegesho kwa namna na viwango
vilivyoainishwa katika Kanuni, endapo mmiliki wa chombo cha usafiri atashindwa kulipa ushuru wa maegesho baada ya Siku 14 tangu alipoondoa chombo cha usafiri katika maegesho, mmiliki huyo atakuwa amekaidi na atawajibika kulipa faini ya shilingi 10,000/=”.

Hivyo, TARURA baada ya kutoa elimu kwa watumiaji wa maegesho kuelewa taratibu za kulipia ushuru wa maegesho Kidigitali imeanza kutumia Kanuni hizo kutoza faini kuanzia leo tarehe 07/04/2022.

Malipo ya Faini ni kwa watumiaji wa maegesho waliolimbikiza madeni ya ushuru wa maegesho ya kuanzia tarehe 01/03/2022 ambapo kutakuwa na mabadiliko kwenye Ankara (Bill) za wateja wenye madeni ya kuanzia tarehe hiyo.

 

Pia, Ikumbukwe kwamba faini inatozwa kwa kila deni la Siku husika lililozidi Siku 14 bila kulipwa.

Mtumiaji wa maegesho unatakiwa kujisajili kwenye mfumo wa maegesho kwa kupiga *152*00# ili kupata taarifa ya Deni pale unapotumia maegesho. Lipia Ushuru wa Maegesho kwa wakati kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala.

 

Pia unaweza kulipa na kuangalia deni kwa kupiga *152*00# au kwa kutumia App ya TeRMIS na GePG zinazopatikana Play Store na App Store “Lipia Ushuru wa Maegesho kwa Maendeleo na Maboresho ya Barabara Zetu”.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano.

Leave a Comment