
HIVI karibuni Global TV ilifanya ziara hadi katika daraja la Mkombozi maarufu kama daraja la Jeshi kujionea changamoto inayoelezwa kuwa inahatarisha usalama wa wananchi wanaotumia daraja hilo.
Daraja hilo ndilo linalounganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani katika eneo la Mpiji Magoe ambako ndiko zinakopakana wilaya za Ubungo na Kibaha.
Wakazi wa eneo hilo wanadai wanapata usumbufu mkubwa sana hasa inapofika msimu wa mvua kutoakana na mto huo kuwa na mamba ambao wanahatarisha maisha yao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkombozi Wilaya ya Kibaha Anasi Abdallah amesema changamoto kubwa ni pale ambapo mto ukijaa maji wakazi wa maeneo hayo wanalazimika kuzunguka njia ya kwenda Kibaha au kulala nje ya miji yao mpaka maji yatakapopungua.
Mwenyekiti huyo anadai mchakato wa kujenga daraja hilo ulianza mwkaa 2000 ambapo kufikia mwaka 2017 daraja likaanza kujengwa hadi kufikia mwaka 2019 likawa limekamilika na kuanza kutumika.
Lakini cha kushangaza ndani ya miaka miwili hadi mitatu daraja hilo limechaka kiasi kwamba linhatarisha uhai wa wananchi wanaolitumia katika shughuli zao za kila siku.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti ni kwamba daraja hilo walipewa msaada kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) ambao kwa pamoja, wakishirikisha na nguvu za wananchi na michango mbalimbali ikiwemo msaada wa Serikali viligharimu jumla ya shilingi milioni 167.
Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu ujenzi wa daraja hilo huku baadhi yao wakitaka uchunguzi ufanyike kwani kuna uwezekano wa kuwepo hujuma.