
ZIARA ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan imechukua nafasi yake ya kipekee baada ya kutokea tukio la kihistoria ambapo kwenye jukwaa walikuwa Rais Samia ambaye ni mwanamke wa kwanza kutawala nchi ya Tanzania pamoja na Kamala Harris Makamu wa Rais wa Marekani ambaye katika historia ya siasa na utawala wa nchi hiyo anakuwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
Katika mazungumzo yao Kamala Harris alitumia nafasi hiyo kuelezea mambo makuu matatu ambayo anatazamia Marekani pamoja na Tanzania watayatekeleza ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo pamoja na uhusiano ulipo baina ya mataifa hayo mawili.
Alisema kuwa Tanzania na Marekani zinatarajia kushirikiana katika Nyanja za Afya, Kilimo pamoja na Miundombinu lakini pia adhima ya kuhakikisha wanaishi kwa kuheshimu misingi ya usawa haki na utawala bora.
Sambamba na hilo viongozi hao wawili waliongelea kuhusu uwekezaji katika sekta ya usafiri wa anga pamoja na uwekezaji wa kiasi cha dola bilioni 1 utakaofanywa na makampuni ya uwekezaji ya Marekani nchini Tanzania.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala aliongelea pia mchango wa serikali yake katika kukabiliana na janga la Uviko-19 nchini Tanzania ambapo Marekani ilitoa msaada wa zaidi ya kiasi cha dola milioni 4.9 kuchangia upatikanaji wa chanjo ya Uviko -19.
Katika mazungumzo yao Kamala alitumia fursa hiyo kukemea uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kusisitiza juu ya nchi zote duniani kushikamana na kuheshimu sheria za kimataifa pamoja na mila desturi pamoja na mipaka baina ya nchi na nchi.
Naye Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania Mark Green ambaye kwa sasa ni Rais wa Kituo cha Kimataifa cha Woodrow Wilson amesema mazungumzo hayo yamekuwa ni ishara ya uhusino mzuri baina ya mataifa hayo mawili lakini pia faida kwa Marekani katika Bara la Afrika.