
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye yupo nchini Marekani katika ziara yake ya kikazi ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha msanii Maunda Zorro kilichotokea eneo la kigamboni kutokana na ajari ya Gari.
Rais Samia ametuma salamu hizo kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka ambaye amesema kuwa Rais Samia amepokea kwa mshituko taarifa za kifo cha Maunda na kwamba anawapa pole wafiwa wote akiwemo baba wa Marehemu pamoja na familia yake kwa ujumla kwani Maunda alikuwa ni kiungo kizuri kwa familia lakini na taifa pia.

Msiba wa Maunda ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wasanii pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, moja ya wasanii waliohudhuria ni pamoja na Kajala Masanja ambaye alimuelezea marehemu kama mtu mwenye roho nzuri enzi ya uhai wake.

“Nikimuongelea marehemu ni mtu ambaye namjua muda mrefu tokea walivyotoka kipindi kile yeye na Mwasiti walikuwa ni kama wadogo zangu kwahiyo msiba huu umenishtua sana, yeye na mwasiti ni watu ambao tulikuwa tunaenda tunashinda nyumbani tunacheka kwahiyo msiba wake umenishitua sana ni mtu ambaye alikuwa akiona kitu chochote kinachonihusu mimi iwe kwenye Media kwenye nini lazima atanitafuta.”
Marehemu Maunda Zorro amezikwa katika makaburi yaliyoko jirani na nyumbani kwake alikokuwa akiishi eneo la Toangoma, Kigamboni jijini Dar es Salaam