
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka watanzania hususa ni Vijana, kuchangamkia fursa za maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Rais Samia ametoa wito huo jijini NewYork nchini Marekani, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati alipozindua Mtandao wa NALA (NALA APP) unaotumiwa na watu waishio Marekani kutuma fedha kwenye nchi za Afrika katika mfumo wa kidijitali.
Alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NALA, Raia wa Tanzania, Bw. Benjamin Fernandes na Timu yake, kwa kubuni Application hiyo ambayo itarahisisha utumaji wa fedha kutoka nchini humo kwenda Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika.

“Benjamin Fernandes na Timu yako ni miongoni mwa vijana wabunifu waliojikita katika masuala ya teknolojia ambao Serikali inawaunga mkono hususan wakati huu ambapo nchi inajenga uchumi wa kidijitali ambao matokeo yake yanatarajwa kuwa ni kukuza ajira, kuchangia pato la Taifa na kukabiliana na changamoto zote za kiuchumi na kijamii” Alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kujenga mkongo wa Taifa uliounganishwa na nchi nyingine za kiafrika zikiwemo Burundi, Kenya, Rwanda, Malawi, Uganda na Zambia na hivi karibuni nchi za DRC na Msumbiji zitaunganishwa.
Dkt. Nchemba alitoa rai kwa wawekezaji kwenye sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuwekeza nchini Tanzania na kufaidi mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo nchi imeweka ili kuvutia mitaji na teknolojia.