×

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

 

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower)

0719401968

“Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!”

“Nanii?”

“Fungua!”

“Jitambulishe kwanza, wewe nani?”

“Nimesema fungua! Fungua kwa hiyari yako!”

“Huyo ni nani?”

“Shiii! Rudi ndani kalale!”

“What is going on? Please let me know!” (Nini kinaendelea? Tafadhali naomba nieleweshe).

“Ngo! Ngo! Ngo!”

Kufumba na kufumbua, kishindo kikubwa kilisikika, mlango ukaja kunibamiza kwa nguvu na kunirusha mpaka ukutani, nikajibamiza na kudondoka chini kama mzigo.

Wanaume watatu waliokuwa wamevalia makoti meusi, walinifuata na kunikaba pale chini huku wakinimulika kwa tochi zenye mwanga mkali usoni.

 

“Tulia, vinginevyo tunakumwaga ubongo sasa hivi,” alisema mmoja kati yao, nikashtuka kusikia akikoki bunduki yake na kuninyooshea.

 

“She is innocent! Please leave her alone!” (Hana makosa! Tafadhali muacheni) nilisema kwa sauti ya kutetemeka, nikashtukia mmoja kati yao akinipiga kwa nguvu kichwani na kitako cha bunduki kisha akanisindikizia kwa kunipiga na buti gumu alilokuwa amevaa, nikasikia kizunguzungu kikali kisha giza nene likatanda kwenye uso wangu, sikuweza tena kuelewa chochote kilichoendelea.

 

Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumepambazuka. Nikakurupuka pale chini nilipokuwa nimelala na kusimama, nikasikia kichwa kikiwa kinanigonga kuliko kawaida. Kilichonishtua ni kwamba pale chini nilipokuwa nimelala, palikuwa na damu nyingi ambazo sasa zilikuwa zimekauka.

 

Nikajishika sehemu mbalimbali za mwili wangu, nikagundua kwamba mdomo wangu ulikuwa umevimba sana, harakaharaka nilisogea kwenye kioo kidogo kilichokuwa ukutani na kujitazama, nikashtuka kwa jinsi nilivyokuwa natisha.

 

Jicho moja lilikuwa limevimba sana na kuweka kama alama za weusi kwa chini yake, mdomo nao ulikuwa hautamaniki. Kwa jinsi ilivyoonesha, ni kwamba wale wanaume walionivamia usiku uliopita, waliendelea kunipiga tena hata baada ya kuwa nimepoteza fahamu.

 

“Lakini kwa nini? Why? Nimefanya kosa gani kwa Mungu wangu kustahili adhabu kali kiasi hiki?” nilijisemea huku nikianza kumwaga machozi. Harakaharaka nikaenda mpaka chumbani, macho yangu yakatua juu ya kitanda, Saima hakuwepo!

 

Nikageuka kutazama huku na kule, nikagundua kwamba hata begi lake pia halikuwepo, uchungu usioelezeka ukanikaba kooni kiasi cha kunifanya nishindwe hata kumeza mate.

 

Nilitoka nje huku nikipepesuka maana maumivu ya kichwa yalikuwa makali sana, nikatazama huku na kule, hakukuwa na dalili yoyote ya kuwepo kwa Saima, nikarudi ndani huku nikiendelea kulia kwa uchungu usioelezeka.

 

Niliwasha moto kwenye jiko la kuni, nikabandika maji na kuchochea mpaka yalipochemka, nikaanza kujikanda maeneo yote yaliyokuwa na majeraha.

 

Nilikuwa nasikia maumivu makali lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo.

 

Nilisukutua mdomo kwa maji yaliyochanganywa na chumvi, maumivu niliyokuwa nayasikia yalikuwa hayaelezeki. Nilijisafisha puani ambako damu ilikuwa imegandia, nikaanza pia kujikanda kwenye jicho.

 

Ama kwa hakika nilikuwa nikisikia maumivu makali sana lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili angalau nipate ahueni.

 

Tangu nifahamiane na Saima, kila kitu changu kilikuwa kimebadilika kabisa na sasa hata usalama wangu wenyewe ulikuwa ni mtihani mgumu.

 

Nasema mtihani kwa sababu kama watu wameweza kujua mahali tulipokimbilia na kujificha, tukiishi maisha kama ya wanakijiji kabisa, lakini watu wameingia mpaka ndani, wamenipiga na kunijeruhi vibaya lakini kama hiyo haitoshi wameondoka na Saima, hiyo ilikuwa ni ishara ya hatari sana kwenye maisha yangu.

 

Sasa kama hata sehemu ya kujificha haipo tena, nini itakuwa hatma yangu? Nilijiuliza maswali mengi sana wakati nikiendelea kujikanda.

 

Baada ya kumaliza kazi hiyo, nilienda kuanza kurekebisha mlango uliokuwa umevunjwa usiku uliopita na watu wale walioondoka na Saima.

 

Niliifanya kazi hiyo huku nikiendelea kujiuliza maswali mengi sana ndani ya kichwa changu. Nilipomaliza, tumbo lilikuwa likitetemeka kwa sababu ya njaa, ikabidi nifanye maarifa ili kutuliza njaa yangu.

 

Kwa bahati nzuri, unga tulionunua mjini na Saima siku tulipoamua kufunga safari kwenda kujificha, bado ulikuwepo.

 

Nikapika ugali harakaharaka na kwa sababu kulikuwa na mboga kidogo tulizobakiza usiku uliopita, sikupata tabu.

 

Baada ya kumaliza kula, nilitoka na kukaa nje, nikawa naendelea kutafakari nini cha kufanya kwa sababu ndani ya muda mfupi tu nilikuwa nimeingia kwenye matatizo makubwa sana ambayo hata sikuwa najua nawezaje kutoka.

 

Uchungu uliponizidia, niliinuka na kuzunguka nyuma ya nyumba yetu, mahali kulipokuwa na makaburi mawili, moja la marehemu baba na lingine la marehemu mama.

 

Nilipiga magoti na kuyainamia, machozi yakawa yananitoka kwa wingi huku uchungu mkali ukizidi kunitesa moyoni mwangu.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia: www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com ,  Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online. Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

 

Leave a Comment