
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Mei, 2022 ameshiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) nchini katika uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma amewahakikishia Wafanyakazi kuwa jambo la nyongeza ya mishahara mwaka huu lipo kama alivyowaahidi mwaka jana na kusema mahesabu yanaendelea ili kujua itapandishwa kwa kiasi gani.

Rais Samia akiongea na Wafanyakazi hao amesema
“Ninakubaliana nanyi kwamba viwango vya mishahara vya sasa havikidhi mahitaji, ili kuendelea kulinda maslahi ya Wafanyakazi, Serikali imeshaunda Bodi za Kima cha Chini cha Mishahara kwa sekta zote na tayari zimeanza kufanya tathmini ili kufanya maboresho
Natumia fursa hii kuwapongeza Watumishi wa sekta zote kwa jitihada na kujitoa kwenu katika kulijenga Taifa letu, bila shaka maendeleo yote yaliyofikiwa tangu nchi yetu ipate uhuru yanatokana na mchango wa Wafanyakazi
Nawashukuru pia kwa kuiunga mkono Serikali yenu katika kuwatumikia Wananchi na kuleta maendeleo nchini, naungana na ATE na ILO katika kuwatia moyo Wafanyakazi kuendelea kuzalisha na kuleta tija kwa maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja na changamoto kadhaa tulizopitia, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tumeweza kupata mafanikio makubwa ikiwemo trilioni 1.49 kutekeleza miradi Sekta ya Elimu, bilioni 234.41 miundombinu ya Afya na bilioni 597 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara.
Pia trilioni 1.4 kwa ajili ya maji Mijini na Vijijini, Aidha, tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo SGR, JNHPP, ununuzi wa ndege 5, ujenzi na upanuzi wa Viwanja vya Ndege na ujenzi wa Bandari

Aidha, kutokana na kuboresha huduma za Wastaafu ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa kielektroniki ambao umeunganishwa na mfumo wa NIDA, malipo ya mafao yameanza kufanyika ndani ya siku 60″
Natambua changamoto za utoaji wa huduma kupitia NHIF, ili kutatua changamoto hizo Serikali imeendelea kuboresha kitita cha mafao ya huduma za afya ambacho hutolewa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya” amesmea Rais Samia

