×

Convoy Protection Jammer, Gari Lenye Uwezo wa Kukata Mawasiliano Kwenye Msafara wa Rais

Convoy Protection Jammer likiwa kwenye msafara wa Rais wa Marekani

KAMA wewe ni mfuatiliaji wa mambo, utakuwa umewahi kuyaona magari fulani hivi meusi, yenye machumachuma na vitu kama antenna kwa juu, kwenye misafara ya viongozi wa juu wa nchi, hususan marais wa nchi mbalimbali.

 

Kama hujawahi, basi nakushauri utazame msafara hata wa Rais Samia Suluhu Hassan, utaliona gari hilo. Wengi huwa wanadhani pengine ni gari la kurushia matangazo na kadhalika lakini ukweli ni kwamba gari hilo lina kazi kubwa na muhimu sana katika ulinzi wa rais.

 

Linaitwa Convoy Protection Jammer, ni gari maalum la kudhibiti mawasiliano ya aina mbalimbali, kuanzia mawimbi ya redio, GSM 2G/3G, GPS Receivers pia simu za satelite. Ina uwezo wakuzuia mawasiliano kwenye mawimbi ya kati ya 20Mhz mpaka 6000 Mhz. Inaweza pia kudhibiti mawimbi ya VHF, UHF, GSM, CDMA, UMTS na kadhalika.

 

Pengine utajiuliza, mawimbi haya yana madhara gani? Ukweli ni kwamba, magaidi au wahalifu, huwa wanatumia mawimbi haya kutegua mabomu yaliyotegwa sehemu fulani kwa kutumia mawimbi ya simu. Yaani bomu linategwa kando ya barabara, pengine porini kabisa halafu anayelipua anakuwa mbali na eneo husika, anasubiri msafara ukifika pale alipotega mabomu tu, anabofya simu yake au rimoti yake kisha bomu linalipuka.

 

Kwa hiyo mitambo iliyopo kwenye gari hili, inafanya kazi ya kuzuia mawimbi ya vilipuzi vya simu au rimoti (mobile activated improvised explosive devices), yasiweze kufika kwenye bomu na kulizuia kulipuka mpaka msafara utakapokuwa umefika umbali fulani.

 

Lakini si hivyo tu, wakati mwingine, yawezekana rais yupo sehemu anahutubia lakini kuna watu wanapanga njama za kumpiga risasi kwa mfano, wanakuwa na watu wao ambao ni miongoni mwa wanaomsikiliza rais, sasa wanachokifanya inakuwa ni kuwasiliana, iwe kwa simu za kawaida au kwa simu za satelite.

 

Kwa kutumia mitambo hii, mawasiliano yanakatwa kabisa na hata kama yakiruhusiwa, maafisa usalama wanakuwa wanasikiliza simu zote zinazopigwa katika eneo kiongozi anapokuwepo kwa kutumia mitambo maalum.

Kwa hiyo utashtukia tu umewekwa ‘mtu kati’ kabla hata ya kutekeleza ulichotaka kukifanya.

 

Sasa yote tisa, kumi ni kwamba Marekani imezindua gari jipya lenye teknolojia ya kisasa zaidi kuliko CPJ zote, linaitwa Mobile Command and Control Vehicle ‘Road Runner’, Ford F350 Super Duty.

Convoy Protection Jammer ikiwa kwenye msafara

Sasa hili ukiacha sifa zote ambazo CPJ za kawaida zinakuwa nazo, lenyewe limeongezewa uwezo wa kuzuia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) na mabomu ya nyuklia kwenye misafara ya Rais wa Marekani, likitumia mawasiliano ya satelite moja kwa moja.

 

Pia lina uwezo wa kuzima mawasiliano yote, kuanzia intaneti na simu za kawaida kiasi kwamba rais akifika mhali, huwezi kupiga simu wala kupata intaneti mpaka atakapoondoka lakini kwa wakati huohuo, inafanya mawasiliano kati ya rais na maafisa wote wa usalama yasiweze kudukuliwa kwa namna yoyote ile.

Leave a Comment