×

Jeshi la Polisi Limefanikiwa Kuwakamata Vijana 31 wa Panya Road

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Murilo Jumanne Murilo

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata vijana 31 wengi wao wakiwa ni wakazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za vitendo vya kihalifu ikiwemo kuiba pesa, TV na baadhi ya vitu vya nyumbani.

 

Vijana hao waliokamatwa wanahusishwa na kuwa vijana wa kundi la Panya Road ambao walianza kutekeleza matukio hayo katika maeneo ya Chanika jijini Dar es Salaam.

 

Akiongea mbele ya Waandishi wa Habari Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Murilo Jumanne Murilo amesema baada ya mahojiano ya kina vijana hao wamekubali kuhusika na matukio hayo na pia wamebainisha mhusika mkuu ambaye amekuwa akiwatuma kutekeleza matukio hayo ya kihalifu.

Vijana 31 waliokamatwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na kundi la Panya Road

Murilo amedai baadhi ya vijana katika kundi hilo walishawahi kukamatwa siku za nyuma kuhusika na matukio ya namna hiyohiyo na wakatumikia adhabu za vifungo vyao lakini pia Murilo ameeleza kuwa vijana hao wamekiri kuwa kabla ya kutekeleza matukio hayo ya kihalifu huwa wanatumia madawa ya kulevya ikiwemo bangi.

 

Kamanda huyo amethibitisha kuwa Jeshi la Polisi limefanikiwa kutia mbaroni mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Saki Hamis (30) mkazi wa Ununio ambaye baada ya kupekuliwa amekutwa na magunia 10 ya bangi kilogram 180 za bangi ambayo ilikuwa haijaandaliwa pamoja na kete 407 kwa ajili ya kuwapatia vijana hao na puli 48.

Leave a Comment