
MBUNGE wa Jimbo la Kibiti mkoani Pwani, Twaha Mpembenwe ambaye hivi karibuni alishusha tani kadhaa za mifuko ya sementi na mabati kwa ajili ya ujenzi wa mashule, zahanati na ofisi za chama jimboni humo, kwa kushirikiana na wahisani wake Kampuni ya PMM Estate (2001) LTD inayojishughulisha na utoaji wa mizigo bandarini jana, alishusha tena mifuko 300 ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za chama jimboni humo.

Mbunge huyo mwenye kauli mbiu ya “Kibiti kwa Maendeleo Inawezekana” ambaye kwenye tukio hiloo aliwaagiza wawakilishi wake amesema ameendelea kumwaga misaada hiyo ikiwa ni ahadi yake kwa wananchi wa jimbo hilo kama alivyowaahidi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliomuingiza madarakani.
Akizungumza kwenye hafla ya kupokea msaada huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibiti na Diwani wa Kata ya Bungu, Ramadhani Mpendu amemshukuru mbunge Mpembenwe na kusema;
“Mbunge huyu amekuwa mhimiri mkubwa sana kwa jimbo la Kibiti ambapo pamoja na leo kutuletea hii mifuko 300 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za CCM lakini kama serikali amekuwa akituunga mkono kwenye mambo mengi sana hapa Kibiti.

“Msaada huu ni juhudi zake binafsi si leo tu amekuwa akituunga mkono kwenye mambo mbalimbali ambapo hivi karibuni halmashauri yetu ilikumbwa na maafa ya kimbunga kwenye maeneo mbalimbali na kuezua mapaa ya maofisi, shule, hospitali, masoko na majengo ya wananchi ambapo mbunge huyo aliweza kutoa misaada sehemu zote hizo na kurudisha mazingira katika hali ya kawaida.

“Mpaka kule Mlanzi alipeleka bati sementi na vifaa vingine vya ujenzi na leo katika kukiimarisha Chama cha Mapinduzi Kibiti ametuletea tena msaada huu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za chama kiukweli sijawahi kuona mbunge kama huyu kwenye jimbo letu”. Alimaliza kusema mwenyekiti huyo wa halmashauri.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibiti Sokoni, ulipokabidhiwa msaada huo, Said Luambo amemshukuru mbunge Mpembenwe kwa msaada huo.

“Ndani ya siku za hivi karibuni hii ni mara ya pili sasa katika eneo hili tunapokea msaada wa kimaendeleo kutoka kwa mbunge huyu msaada uliopita tulipokea sementi mifuko 600 kwa ajili ya maendeleo ya wanakibiti na sasa mifuko 300 Mungu azidi kumbariki yeye na wahisani wake”. Alimaliza kusema mwenyekiti huyo.
Akizungumza baada ya hafla hiyo mwakilishi wa Kampuni ya PMM Juma Hugo amesema kampuni yake imeleta sementi hiyo kwa mbunge wa Kibiti ambayo ataitumia kwaajili ya maendeleo ya jimbo lake.