
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa, licha ya Serikali kufanya kazi nzuri katika sekta anayoisimamia lakini bado kuna changamoto ambazo zinahitaji mjadala wa pamoja wa wadau ili kuzipatia ufumbuzi.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo kwenye mazungumzo na Katibu wa Bunge wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Mhe. Robert Oliphant yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 26 Mei 2022. Mhe. Nape alieleza kuwa uhuru wa kujieleza ni moja ya haki ya msingi ya mwanadamu ambayo haipaswi kuingiliwa kwa namna yeyote, isipokuwa tatizo linajitokeza, pale matumizi ya haki hiyo yanapoharibu haki ya faragha ya mtu mwingine, pasi na kuwa na mipaka inayotenganisha haki hizo mbili.

Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri Nape alisisitiza umuhimu wa Canada na wadau wengine kushirikiana na Serikali kuwa na mjadala utakaoweka vigezo vya mipaka ya uhuru wa kujieleza usioharibu haki ya mtu mwingine. Kiongozi huyo alieleza kuwa sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni muhimu katika maendeleo ya nchi, kwa kuwa ni mtambuka na inasaidia katika utoaji wa huduma bora na kwa haraka katika sekta nyingine kama za Kilimo, Elimu, Afya na Fedha. Hivyo, ameiomba Canada kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye TEHAMA hapa nchini.
Kwa upande wake, Mhe. Oliphant alieleza kuwa Canada imeamua kubuni mkakati maalum wa kushirikiana na nchi za Afrika na kutokana na mkakati huo ametumwa na Serikali yake kuja Tanzania kuangalia maeneo ambayo nchi hizi mbili zinaweza kushirikiana kwa faida za pande zote mbili. Aliahidi kuwa, ujumbe wa wafanybiashara kutoka Canada utatembelea nchini ili kuangalia maeneo ya uwekezaji kwenye sekta ya TEHAMA.
Kuhusu kilimo, Kiongozi huyo alisema kuwa Serikali ya Canada imetoa Dola za Canada milioni 100 kuipa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuendeleza kilimo barani Afrika. Ameshauri kuwa Serikali ya Tanzania inaweza kuchangamkia fursa hiyo ambayo inalenga zaidi wakulima wadogo na wakati.

Kiongozi huyo wa Canada ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 25 Mei 2022, amefanya mazungumzo pia na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk (Mb.), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bibi Mary Makondo.
Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri Gwajima alielezea dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa masuala ya usawa wa kijinsia yakiwemo kuwajengea uwezo wanawake; kuondoa unyanyasaji wa kijinsia na kuwawekea mazingira mazuri makundi maalum kama vile vijana, watoto, wamachinga, wazee yanapewa kipaumbele katika Serikali yake.
Balozi Mbarouk kwa upande wake alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Canada ni mzuri na kusisitiza umuhimu wa uhusiano huo ujikite zaidi katika biashara na uwekezaji. Alisema licha ya uwepo wa kampuni za Canada zilizowekeza nchini, kuna umuhimu wa nchi hiyo kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kwani Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo hazijatumika. Aidha, Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa Wizara kufanya kazi kwa pamoja na Ubalozi ili kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya watalii kutoka Canada kuja nchini na kuharakisha upatikanaji wa viza kwa wanafunzi wa Tanzania wanaokwenda kusoma Canada.
Wakati wa mazungumzo na Mgeni huyo, Bibi Makondo alimweleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara yake ambazo kiujumla zilionesha namna Serikali ya awamu ya sita ilivyojipanga kuhakikisha kuwa inatenda haki kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi. Aliishukuru Canada kwa misaada inayotoa hususan kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambayo imewezesha wakala huyo kutekeleza majukumu yake kwa kiwango cha kuridhisha. Mhe. Oliphant aliwaeleza viongozi hao kuwa Canada itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania kutokana na msimamo wa Rais amia Suluhu Hassan wa kuonesha dhamira ya dhati ya kufanya
mabadiliko makubwa kwenye Uchumi, Utawala wa Sheria, Demokrasia na Haki za Binadamu.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki