
KANSELA wa Ujerumani Olaf Scholz amekutwa katika hali ya mshangao baada ya kuzomewa na wananchi wa mji wa Dusseldorf kutokana na kitendo chake cha kushindwa kutoa msaada wa zana za kivita nchini Ukraine.
Scholz amekuwa akikosolewa na jumuiya za kimataifa hasa wanachama wa NATO kutokana na kusita katika kutekeleza ahadi yake ya kuiynga mkono Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Rais wa Poland Andrzej Duda amenukuliwa akisema Berlin ilitoa ahadi ya kusaidia kupeleka vifaru vya kisasa maarufu kama Vifaru Chui (Leopard Tanks) ambavyo vingeweza kwenda kuchukua nafasi ya vifaru vya enzi za kisovieti vilivyopelekwa nchini Ukraine lakini hadi sasa Ujerumani haijatekeleza ahadi hiyo na haionekani kutekeleza.
Kansela Scholz ambaye anatoka kwenye Chama cha Social Democrat SPD amesema kwa kutoa zana hizo mpya za kivita kwa Ukraine haitakuwa na msaada wowote zaidi hasa itakuwa ni kuchochea vita hiyo.

Kwa sasa Ujerumani mbali na kutoa misaada ya zana za kivita kwa nchi ya Ukraine lakini pia inatoa mafunzo maalum kwa askari wa Ukraine katika eneo la Panzerhaubitze.
Hadi sasa Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani Annalena Baerbock ametembelea Ukraine lakini Kansela Scholz hajatembelea nchi hiyo huku akishutumiwa kuwa mmoja ya watu wanaokwamisha juhudi za Ukraine katika kukabiliana na mashambulizi ya Urusi.

Kwa muda mwingi Scholz amenukuliwa akiwa akisema kuwa kutembelea nchini Ukraine na kuishia kupiga picha za kushikana mikono hakuna faida yoyote, ingawa amekuwa akinukuliwa kwa kauli yake ya kuwa Putin hatakiwi kushinda ingawa hasemi kuwa Ukraine inatakiwa kushinda vita hiyo.