×

Wanaovaa Nguo Fupi Wakamatwa,Wapigwa Faini Mifuko Mitano ya Saruji

Wananchi wa Makete mkoani Njombe

KATIKA jambo ambalo sio la kawaida, kumeibuka mjadala mzito kwa baadhi ya wananchi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe mara baada ya baadhi ya maeneo yenye mamlaka kiutawala kutunga sheria ndogo zinazotajwa kuwa ni maumivu kwa wananchi.

 

Hali hiyo imeibuka mara baada ya uongozi wa kata ya Tandala wilayani humo kupitia vikao vyao vya kata (KAMAKA) kutunga sheria ndogo ya kuwakamata wanawake wanaovaa nguo fupi,nguo zinazochora maumbile yao pamoja na wanaume wanaovaa suruali zikiwa chini ya makalio (Mlegezo) na kuwapiga faini ya mifuko mitano ya saruji inayokwenda kutumika kwenye ujenzi wa miradi ya kata.

 

Mtendaji wa kata hiyo bwana Maximilian Msigwa amesema uamuzi huo umefanyika ili kudhibiti mavazi yasiyofaa katika jamii na kubainisha kuwa mpaka sasa umekwishafanyika msako na tayari baadhi ya watu ambao idadi yao haijafahamika wakiwa wamekwishakamatwa katika utekelezaji wa sheria hiyo.

Ukivaa nguo fupi Makete, faini mifuko mitano ya saruji

“Tumekuwa na mabinti wengi wanaokuja kutafuta riziki sasa wanakuja kutafuta kwa njia tofauti sasa wanapokosea lazima tuwanyooshe warudi kwenye mstari,akiweza kukamatwa analipishwa mifuko mitano ya saruji kwa ajili ya ujenzi kwasababu tuna ujenzi wa shule yetu ya msingi Tandala”alisema Maximilian Msigwa.

 

Msigwa amesema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo wamiliki wa sehemu za starehe na wananchi kwa ujumla walipewa taarifa kwa ajili ya kujirekebisha kabla sheria hiyo haijaanza kufanya kazi na kuongeza kuwa wote wanaoshindwa kulipa gharama hizo kumewekwa utaratibu wa kuzungumza na viongozi wao wa vijiji ili kuwatambua na kuwarudishwa kwao.

Leave a Comment