×

Waziri wa Nishati Awasilisha Bajeti Yake Bungeni, Agusia Maboresha ya Umeme Vijijini

Waziri wa Nishati January Makamba

WAZIRI wa Nishati January Makamba ametoa hotuba ya makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye Bunge Kuu la Bajeti linaloendelea jijini Dodoma.

 

Katika Hotuba yake Waziri Makamba amegusia mambo mbalimbali ikiwemo wananchi wanaoishi Mijini lakini maeneo yao yana sifa za vijiji ambao kimsingi wamekuwa wakiilalamikia Serikali juu ya gharama za kuunganisha umeme ambazo zinakuwa za juu tofauti na hali zao za uchumi.

 

Waziri Makamba katika ufafanuzi wake amesema tayari ameshaunda timu inayojumuisha Wizara ya Nishati, TANESCO pamoja na REA itakayokuwa na jukumu la kuzunguka miji yote nchini na kubaini maeneo hayo kwa kuwashirikisha Wabunge wa maeneo husika.

 

Waziri Makamba amebainisha kuwa maeneo yote yatakayoainishwa na timu hiyo basi yatajumuishwa kwenye bei ya vijijini ambayo ni shilingi 27,000 na zoezi hilo linatarajiwa kufanyika ndani ya muda wa miezi sita (6).

Waziri Makamba amewasilisha Bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/2023

Makamba pia amesema kwa kuzingatia mwenendo wa bajeti kila mwaka ya kupeleka umeme vijijini, itachukua zaidi ya miaka 15 kufikisha umeme katika vitongoji vilivyosalia. Kwa muktadha huo, Serikali  itahakikisha rasilimali fedha inapatikana ili kufikisha umeme katika vitongoji vyote.

 

Kuhusu Nishati ya Gesi, Serikali ilitenga vitalu vya mafuta na gesi vya kimkakati kwa ajili ya kuipatia TPDC ili kuijengea uwezo na uzoefu. Vitalu hivyo ni Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi-Wembere, Songosongo Magharibi. Ziwa Tanganyika na 4/1B na 4/1C. Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali imetenga kiasi kwa shilingi bilioni 102.167 kwa ajili ya kazi mbalimbali za maandalizi ya uchimbaji wa gesi na mafuta kwenye vitalu hivyo.

 

Waziri Makamba amebainisha kuwa, Serikali ina makubaliano ya awali na nchi za Uganda na Kenya kwa ajili ya ujenzi wa mabomba ya kusafirishia gesi asilia kutoka Tanzania kwenda kwenye nchi hizo.

 

Miradi yote ipo katika hatua za awali, ikiwemo matayarisho ya kufanya upembuzi yakinifu.

 

Kwa upande wa mradi wa bomba la kwenda Uganda, Serikali imetenga shilingi milioni 635 na upande wa bomba la kwenda Kenya shilingi milioni 656.10 kwa ajili ya kazi mbalimbali za awali.

Leave a Comment