
MWANAMUZIKI Mkongwe wa Dansi aliyewahi kutamba na kundi la Twanga Pepeta Khadija Kimobitel amesema tayari amefanikiwa kununua vyombo pamoja na kukusanya wanamuziki na hadi sasa anarekodi nyimbo kwa ajili ya kuzindua rasmi Bendi yake.
Kimobitel amebainisha hayo katika kipindi cha Express Afrika kinachorushwa na +255Global Radio na Global TV ambapo ameendelea kubainisha kuwa mazoezi yanafanyika maeneo ya Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es Salaam na mpango wake ni kuzindua Bendi na nyimbo mpya kwani hadi sasa ana jumla ya nyimbo tatu ambazo zinaandaliwa Studio.
Mwanamuziki huyo aliyetamba kwa kuimba na kunengua amesema uhusiano wake na wanamuziki wenzake wa zamani kutoka kundi la Twanga Pepeta akiwemo Ally Choki ni mzuri na anadhamiria kusimama yeye mwenyewe kuendesha Bendi yake hiyo mpya.

Amelitaja jina la Bendi yake kuwa ni Kimo Kimo Bendi akiwa jina ambalo anadai alipewa na Marehemu Banza Stone enzi za uhai wake.
Alipogusiwa kuhusu kuwekeza katika mitandao ya kijamii kama wanavyofanya wasanii wa sasa wa Bongo Fleva alisema kwa sasa yeey hicho siyo kipaumbele chake kwani bado hajaandaa Menejimenti nzuri ya kusimamia kazi zake katika upande huo.