
SERIKALI ya Zimbabwe imekanusha madai yanayoenea kwamba raia wake wamekuwa wakiuza baadhi ya vidole vyao vya miguu ili kupata mamilioni ya pesa.
Naibu Waziri wa Habari wa nchi hiyo, Kindness Paradza ameyataja madai hayo kuwa ni batili na kuwasihi watu kuyapuuza.
“Tulifanya utafiti juu ya suala hili na tukagundua ni uongo. Hizi ni taarifa za mitandao ya kijamii zinazolenga kuchafua jina la nchi,” alisema Paradza.
Mbunge huyo aliongeza kuwa amejipa jukumu la kuzuru Ximex Mall na kuwahoji wafanyabiashara waliokanusha madai hayo na kuongeza kuwa kumekuwa na wimbi la watu wanaotembelea maduka hayo tangu hadithi hiyo iliposambazwa, baadhi yao wakitoka vijijini umbali wa kilomita 80.
Kwa mujibu wa gazeti la The Herald la nchini humo, mtu anayedai kuhusika na biashara hiyo amefafanua kuwa alitoa matamshi hayo alipokuwa amelewa.

Habari hizo zilienea kwenye mitandao ya kijamii baada ya watu kadhaa kusambaza picha zao wakiwa kwenye magari ya kifahari wakidai kuwa wameyanunua magari hayo kutokana na kuuza vidole vya miguu.
Katika moja ya video hizo, mwanaume mwenye umri wa makamo alionekana akiwa ameweka mkono kwenye gari mpya aina ya Range Rover huku mwanaume mwingine akiwa tayari kumkata vidole vidogo vya miguu.
Madai hayo yalichochewa zaidi na blog iliyosema kuwa mnunuzi huyo alikuwa katika eneo la Ximex Mall katika mji mkuu wa Zimbabwe wa Harare.
Alipoulizwa kwa nini yeyote aliyekuwa akinunua vidole hivyo alivihitaji, ripoti hiyo ilionyesha kuwa vilitumika kwa matambiko nchini Afrika Kusini.
Kulingana na taarifa za watu waliohusika na madai hayo, kidole gumba cha mguu kina thamani ya $40,000 (Tsh milioni 93), kidole cha kati ni $25,000 (Tsh milioni 58) huku kidole kidogo kikipata $10,000 (Tsh milioni 23).