
RAIS wa Marekani Joe Biden ametangaza hatua maalum ya nchi yake katika kuhakikisha usalama wa mataifa ya Ulaya hasa yale ambayo yapo katika Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi NATO.

Rais Biden ametanabaisha kuwa atatuma majeshi yake katika nchi hizo ili kuzisaidia katika harakati za kukabiliana na vitisho vya mashambulizi ya nchi ya Urusi.
Wakuu mbalimbali wa nchi za Umoja wa kujihami wan chi za magharibi NATO wapo jijini Madrid wakiendelea na mkutano wao wa mwaka ambao ajenda kuu imekuwa ni kujadili namna gani ambavyo mataifa ya NATO yanaweza kukabiliana na uvamizi au hatari ya mashambulizi ya Urusi kwa nchi wanachama.

Katika mkutano wake na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, Rais Biden amethibitisha kuwa adhima ya Marekani ni kuona dunia inakuwa na Amani na utulivu pamoja na demokrasia ya kweli yenye utawala bora lakini pia amesema Marekani itahakikisha inazindua Ngome ya kudumu ya Kijeshi nchini Poland na kupeleka ndege ya mapigano ya kijeshi aina ya F-35 nchini Uingereza huku ikiimarisha ulinzi na zana nyingine nchini Ujerumani na Italia.
Aidha Rais Biden amesema ataongeza Brigedi moja nchini Romania yenye vikosi ya 5,000.
;