
Wabunge nchini Sri Lanka wamefikia muafaka wa kumchagua rais mpya wa nchi mapema wiki ijayo lakini, licha ya kufikia muafaka huo bado kumekuwa na mvutano mkubwa juu ya kuamua muundo wa serikali mpya ili kuiondoa nchi hiyo iliyofilisika kutoka katika anguko la kiuchumi na kisiasa.
Wabunge hao wa Bunge la Sri-Lanka wamekubaliana kumchagua rais mpya kutoka miongoni mwao mapema ifikapo Julai 20 lakini bado hawajaamua juu ya kiongozi atakayechukua nafasi ya waziri mkuu ili kulijaza baraza la mawaziri ambalo litaunda serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Rais mpya atahudumu kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Gotabaya Rajapksa, ambao unakamilika mwaka wa 2024 na huenda akamteuwa waziri mkuu mpya, ambaye kisha atahitajika kuidhinishwa na Bunge.
Rajapaksa aliahidi kujiuzulu wadhifa wa rais kesho huku Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe akisema ataondoka madarakani mara baada ya kuundwa serikali mpya ya mpito.
