
MSAIDIZI Mkuu wa Rais wa Uturuki amesema kuwa jumuiya ya kimataifa haiwezi kumaliza vita nchini Ukraine kwa kuipuuza Moscow.
Amesema hayo wakati Erdon na Putin wakijiandaa kukutana, katika mkutano wa ngazi ya juu unaokuja baada ya Uturuki kusaidia kupata makubaliano ya kurejesha mauzo ya nafaka ya Bahari nyeusi ya Ukraine ambayo ilikuwa imezuiliwa na uvamizi wa Urusi.
Mkurugenzi Mkuu wa mawasiliano wa Rais wa Uturuki Fahrettin Altun, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba makubaliano hayo yanathibitisha mafanikio makubwa ya Uturuki katika juhudi za kuirejesha amani kati ya Ukraine na Urusi huku akikosoa nchi nyingine zinazochochea vita kuendelea.

Kiongozi huyo wa Uturuki alinukuliwa akisema:
“Ukweli ni kwamba baadhi ya marafiki wetu hawataki vita iishe wanamwaga machozi ya Mamba, Jumuiya ya kimataifa haiwezi kumaliza vita nchini Ukraine kwa kuipuuza Urusi, Diplomasia na amani lazima vitawale.”

Alimaliza kwa kusema kuwa baadhi ya Watu walikuwa wakijaribu kudhoofisha juhudi za Uturuki bila mafanikio, lakini hakutaja watu hao ni akina nani.
Ikumbukwe kuwa katika siku chache zilizopita Uturuki imesaidia katika kusainiwa kwa Mkataba mpya Mjini Istanbul Unaoiruhusu nchi ya Ukraine kuuza nafaka yake nje ambapo Meli ya kwanza kutoka Ukraine ikibeba mahindi imeelekea nchini Lebanon.