
TAASISI ya Wananchi Wazalendo Tanzania (TWWT) chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Ezekiel Kyogo ambaye pia Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi ya Kariakoo imeendelea kusambaza elimu ya kizalendo kwa Watanzania ambapo wikiendi hii imetoa elimu hiyo kwa vijana zaidi ya 400 wa Kanisa la EAGT la Sekondari ya Pugu, Dar.

Katika mkusanyiko pamoja na Dkt. Kyogo viongozi wengine waliotoa elimu hiyo kwenye umati huo uliofurika ni viongozi wa kidini akiwemo Mkurugenzi wa CGM Kanisa la EAGT Jimbo la Ilala, Jeremia Dismas na Mchungaji Mpeli Alick wa Kanisa la EAGT Tabata na Makamo askofu Jimbo la Ilala. Akizungumza na umati huo Dkt Kyogo alisema;

“Wananchi tunapokuwa wazalendo tunawasaidia hata viongozi wetu wanaoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Afande IGP, Camilius Wambula na wasaidizi wake wenye jukumu la kulinda usalama wa nchi.

Kuna watu wengine hawana uzalendo hata kidogo unakuta mtu anamuona mwenzake anafanya uhalifu lakini yeye anashindwa kufichua huo uhalifu na kusema siyo kazi yake, huo si uzalendo kusema kweli na tukiendelea hivyo tunaweza hata kuona wageni wanakuja kuhujumu nchi yetu na kuwaangalia tukisema sisi haituhusu hiyo si sahihi kwakweli”. Alisema Dkt. Kyogo.

Baada ya mkutano huo umati ulionekana kujawa na roho ya kizalendo na kuahidi kuifanyia kazi elimu waliyopewa na kuahidi kusambaza elimu hiyo kwa wengine ambao hawakuweza kufika kwenye mkutano huo.