
RAISI wa Ukraini Volodymyr Zelenskyy ameuonya ulimwengu kwamba Urusi ina mpango wa kufyatua kinu kikubwa cha nyuklia barani ulaya (Zaporizhzhia) kilichopo kusini mashariki mwa Ukraine.
Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia Alhamisi, Zelensyy aliitaka Urusi irejeshe mtambo huo chini ya udhibiti wa Ukraine na kusema “ulimwengu unapaswa kuchukua hatua mara moja kuwafukuza wavamizi” kutoka katika eneo karibu na kituo hicho.

Zelenskyy aliendelea kwa kusema “Urusi kwa mara nyingine tena ilivunja historia ya ugaidi ulimwenguni, Hakuna mtu mwingine aliyetumia mtambo wa nyuklia, kwa hivyo ni wazi anatishia ulimwengu mzima na kila mtu ulimwenguni anapaswa kujibu mara moja kwa kuwafukuza watoke katika eneo la kiwanda cha nguvu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, Hii ni kwa maslahi ya ulimwengu mzima na si ukraine pekee.”
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Energoatom la Ukraine ilisema jengo la Zaporizhzhia lilishambuliwa mara tano siku ya Alhamisi, ikiwa ni pamoja na karibu na mahali ambapo vifaa vya mionzi huhifadhiwa huku Moscow na Kyiv zikilaumiana kwa mashambulizi hayo.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za kijeshi karibu na Zaporizhzhia.

Katika taarifa yake kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioitishwa na Urusi, Katibu Mkuu Antonio Guterres alionya kwamba uharibifu wowote unaweza kusababisha “matokeo mabaya katika eneo hilo na kwingineko, kituo hicho hakipaswi kutumika kama sehemu ya operesheni yoyote ya kijeshi Badala yake, makubaliano ya haraka yanahitajika ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo,” Guterres alisema katika taarifa.
Pia alizitaka Urusi na Ukraine kuruhusu mara moja wataalam wa nyuklia kufikia mtambo huo ili kutathmini uharibifu na kutathmini usalama.