
IKIWA ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imetangaza nafasi za ufadhili wa masomo ya kilimo kwa vijana wa Kitanzania wanaotoka kwenye familia zenye kipato duni.
Ufadhili huo unaotolewa kila mwaka, Hunatolewa chini ya program ya SBL inayojulikana kama Kilimo Viwanda ambapo wanufaika hulipiwa gharama zote za masomo na kwa kipindi chote wanachokuwa masomoni.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa dirisha la maombi kwa mwaka huu, mkurugenzi mtendaji wa SBL Mark Ocitti alisema program hiyo imekuwa ikisaidia kuunga mkono jitihada za serikali za kuzalisha wataalamu wapya wa kilimo ambao ni chachu muhimu katika kuwasidia wakulima kuongeza tija katika kilimo chao.
“Leo hii tunayo furaha kusimama na kusema kuwa program hii imeweza kuwanufaisha vijana wa kitanzania zaidiya 200. Baadhi yao wamepata fursa ya kujifunza zaidi kwa vitendo kwenye viwanda vyetu. Lengo letu ni kuona kuwa program hii inakuwa na matokeo chanya kwa sekta ya kilimo na kwa vijana wanaonufaika nayo pia,” alisema.

Emmanuel Ntandu ambaye ni mnufaika wa program hiyo kutoka chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole Wazazi kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani na ambaye amepata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika kiwanda cha Dar es Salaam alisema “Naishukuru sana kampuni ya SBL kwa kunipatia fursa ya kujifunza zaidi kwa vitendo katika kiwanda chake cha Dar es Salaam kupitia progamu ya Kilimo Viwanda. Nimejifunza mambo mengi na bado naendelea kujifunza.”
Programu ya Kilimo viwanda ilianzishwa na SBL mwaka 2019 ikilenga kusaidia kuongeza wataalamu wa kilimo kupitia kutoa ufadhili wa masomo. Wanufaikawa program ni vijana wa Kitanzania wenye ufaulu mzuri darasani na ambao wanatokea katika familia zenye kipato duni.

Katika utekelezaji wa programuhii, SBL imeingia ubia na vyuo vine vya ndani vinavyofundisha fani ya kilimo ambavyo hupokea wanafunzi wanaolipiwa kupitia programu hii.
Vyuo hivyo ni Pamoja na Chuo cha Kilimo na Mifugo Kaole Wazazi kilichopo Bagamoyo Pwani, Chuo cha Kilimo na Mifungo cha Kilacha kilichopo Moshi Kilimanjaro, Chuo cha Kilimo Mt. Maria Goretti kilichopo Iringa na chuo cha Kilomo Igabiro kilichopo Muleba mkoani Kagera.