
KUFUATIA kifo cha aliyekuwa Rais wa Urusi na mwanasiasa mkongwe ambaye anakumbukwa na mataifa ya magharibi kwa kumaliza vita baridi baina ya Ulaya Mashariki na Ulaya Magharibi Mikhail Gorbachev, mamia ya waombolezaji wamejitokeza kutoa heshima zao za mwisho ingawa Rais wa sasa wa nchi hiyo Vladimir Putin hajatokea.
Taarifa kutoka Kremlin zinadai kuwa Rais Putin ameshindwa kuhudhuria tukio hilo kwa kukosa muda kutokana na kuwa na majukumu mengi ya kiserikali.

Duru za kisiasa zinadai kuwa kabla ya kufariki kwake Gorbachev hakuwa na uhusiano mzuri na Rais wa sasa wa Urusi Vladimir Putin kutokana na kulaumiwa kuwa moja ya watu walioiletea Urusi matatizo makubwa ya kiuchumi baada ya kushindwa kuzuia anguko ya USSR mnamo mwaka 1991 kwani imebainishwa kuwa mara ya mwisho Gorbachev kuonana ana kwa ana na Putin ilikuwa ni mwaka 2006.

Nje ya Urusi hasa katika mataifa ya Ulaya Magharibi pamoja na Marekani, Mikhail Gorbachev anasifika kwa kuwa kiongozi wa aina ya kipekee kwani aliweza kutatua mgogoro wa vita baridi ambao ulisaidia kutengeneza mlengo sahihi wa siasa za Bara la Ulaya.

Mnamo mwaka 1990 Gorbachev alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kama ishara ya kutambua mchango wake katika kurekebisha mlengo wa siasa na uhusiano wa nchi za Ulaya Mashariki na Magharibi