×

Jaji Mstaafu Othman Chande Asema Watanzania Wasihofie Kubadili Katiba

Jaji Mstaafu Othman Chande

JAJI Mkuu wa mstaafu wa Tanazania, Mohammed Chande Othman amewataka Watanzania wasiwe na hofu ya kufanya mabadiliko ya Katiba yatakayoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani kama inavyofanya Kenya na baadhi ya nchi za Afrika.

 

Amesema Tanzania isiofie kuhusu mabadiliko yatakayoruhusu jambo hilo, bali ijiandae kuwa na demokrasia, uwazi na uwajibikaji katika chaguzi mbalimbali zitakazofanyika.

 

Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekipa jukumu Kikosi Kazi cha kukusanya na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia, hoja ya Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi ndivyo vimetawala zaidi katika maoni yaliyowasilishwa na wadau kwenye Kikosi Kazi hicho.

 

Jaji Chande ameshauri mabadiliko ya Katiba yatakayoruhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani kwa kuwa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ibara 41 (7) inaeleza kuwa “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka yakuchunguza kuchaguliwa kwake.

Jaji Chande amesema Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya Katiba

Jaji Chande ambaye alikuwa kiongozi wa Jukwaa la Majaji na Wanasheria wa Afrika waliokwenda nchini Kenya, kuangalia mwenendo wa kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022, alisema kuna mambo ya msingi ambayo Tanzania inapaswa kujifunza kutoka Kenya.

 

Wito huo ameutoa jana  wakati akigusia masuala mbalimbali yaliyojiri katika uchaguzi na kesi ya kupinga matokeo ya kura za urais wa Kenya iliyotolewa uamuzi juzi.

 

Juzi Mahakama ya Juu ya Kenya ilithibitisha ushindi wa Dk William Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza baada ya kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wake iliyofunguliwa na mpinzani wake mkuu Raila Odinga na baadhi ya watu ambao walidai kulikuwa na udanganyifu na udukuzi wa mifumo ya kusafirisha na kujumlisha kura.

 

Katika maelezo yake Jaji Chande, alisema Tanzania na nchi nyingine za Afrika zina mengi ya kujifunza kutoka Kenya kuhusu demokrasia, uwazi, uhuru wa mahakama, mwenendo wa uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi ambavyo vimewezesha kufanyika kwa uchaguzi wa amani na utulivu

 

“Matokeo ya urais kupingwa mahakamani si hoja ngeni wala haipaswi kuhofiwa na Watanzania, ni suala la kukuza demokrasia, uwazi na utawala wa sheria.Lina mantiki kubwa kwa ustawi wa watu”

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

“Kwa Afrika Mashariki Kenya na Uganda imewezekana. Katiba zao zinaruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani si tu na wagombea bali na mwananchi yoyote, hivyo hivyo Afrika Kusini na Malawi nazo zimeruhusu jambo hilo, hivyo Watanzania hatuna sababu ya kuhofia, nashauri tujiandae” alisema.

 

Alisema haoni sababu ya Tanzania kuhofia matokeo ya kura za urais kuhojiwa mahakamani kwa kuwa siku za usoni kutakuwa na Mahakama ya Juu iliyopendekezwa katika rasimu ya mabadiliko ya Katiba na pia ikaridhiwa na Bunge Maalumu lililotoa Katiba inayopendekezwa.

 

Imeandikwa na Oswald Mwesiga kwa msaada wa mitandao

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Comment