
DAR ES SALAAM 16 Septemba 2022: Mtandao wa jinsia nchini TGNP kwa kushirikina na shirika la WiLDAF umeendelea kushirikiana na vyama vya siasa katika kuboresha sera za vyama hivyo ili viwe na sera yenye mrengo wa Kijinsia ambapo jana Alhamisi majadiliano hayo yalifanyika Makao Makuu ya Chama cha ACT Wazalendo kilichopo Kijitonyama kwa ajili ya kutunga sera ya jinsi kwa chama hicho.

Akizungumza na mwanahabari wetu jana Alhamisi kikao cha uboreshaji sera hiyo, Mwezeshaji na Mwelekezi kutoka TGNP, ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Dkt. Consolata Sule amesema lengo kuu la mijadala hiyo ni kutengeneza sera bora ya kijinsia. Aliendelea kusema;

“Sera hii inatengenezwa kwa kushirikiana na taasisi Mtandao wa TGNP ambao unafanyakazi na wataalamu wengine ili kusaidia vyama vya siasa kuwa na sera ya jinsia.

“Lengo la mpango huu ni kuhakikisha vyama vinafanya michakato yake ya ndani na kuandaa viongozi wa kitaifa kulingana na usawa wa jinsia katika nchi yetu”. Alisema Dkt. Consolata.
Kwa upande wake Katibu wa Maadili wa chama hicho, Kuruthum Jumanne amesema anaishukuru TGNP na Shirika la WiLDAF kwa kuwaandalia mpango wa kufanya maboresho ya sera ya jinsia katika vyama vyetu.
Kuruthum amesema anaamini mpango huu utawamsha wanawake na watu wenye uhitaji maalum kushiriki kwa wingi sawa na wanaume kwenye harakati za kisiasa kwa kuona sasa kuna sera inayowalinda na wao kupata nafasi za uongozi.
Kwa upende wake Idrisa Koeta ambaye ni Katibu wa Sera Utafiti na Mafunzo Taifa ameipongeza TGNP kwa kuwaongoza kwenye mpango huu wa uandaa wa sera ya jinsia kwenye chama chao. Idrisa amesema mpango huu utakuwa ukombozi kwa wanawake na watu wenye uhitaji maalum ambao walikuwa wakihofia kujihusisha kwenye masuala ya kisiasa kutokana na jinsi walivyo.