×

Mch. Masanja awataka viongozi kuwa kioo cha jamii

MSHAURI wa masuala ya itifaki na uongozi bora, Mchungaji Emmanuel Masanja, amewataka viongozi kufanya mambo yenye maadili wakiwa mwangani au gizani kwa kuwa wao ni kioo cha jamii.

 

Mchungaji Masanja ameyasema hayo wakati akifundisha katika semina ya uongozi bora na itifaki kwa viongozi mbalimbali wa kanisa na taasisi iliyofanyika jana Jumamosi kwenye Ukumbi wa Consolata Mission, Bunju jijini Dar es Salaam.

 

Mchungaji Masanja alisema kila anachokifanya kiongozi iwe mwangani au gizani kinafuatiliwa na wale anaowaongoza, hata kama amejificha.

 

 

“Kila kitu chako kinafuatiliwa. Ni vizuri kwa kiongozi kuwa kioo. Kuishi katika maadili na kuwa mfano bora wa kuigwa,” alisema Mchungaji Masanja.

“Mtu asiudharau ujana wako. Kiongozi usiwe mropokaji. Ni lazima kiongozi ujue wakati sahihi wa kusema na wakati sahihi wa kutokusema.

 

“Unaweza ukawa na kitu kizuri cha kusema lakini kwa sababu siyo wakati wake ukaharibu zaidi badala ya kutengeneza.

 

“Ni lazima uzitatue changamoto kwa hekima. Usimamie maamuzi yaliyoamuliwa katika vikao halali kwa hekima. Mavazi unayovaa lazima yakuonyeshe kwamba wewe ni kiongozi,” alisema Mchungaji Masanja.

 

 

Leave a Comment