
MTAALAM wa ushauri wa mambo ya uongozi, utawala na menejimenti, Mchungaji Dk. Joseph Mayala, ametaja mambo matano ambayo kiongozi anatakiwa kuwa nayo ili kufikia malengo ya taasisi au jamii anayoiongoza.
Akizungumza katika semina ya viongozi mbalimbali wa kanisa, jamii, taasisi na kada mbalimbali iliyoandaliwa na Kanisa la AICT Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Dk. Mayala alisema kiongozi anatakiwa kuwa na utambulisho, maono, huruma, uhusiano mzuri na imani ya kufanikisha malengo.
Katika semina hiyo iliyofanyika jana Jumamosi kwenye Ukumbi wa Consolata Mission, Bunju jijini Dar es Salaam, Dk. Mayala ambaye anamiliki taasisi ya Good Works inayojishughulisha na kutoa ushauri wa kiuongozi na utawala kwenye taasisi mbalimbali za kijamii, alisema: “Kwenye utambulisho ndiyo kile kinachoitwa CV – wewe ni nani? Jina, umri, makazi, hali ya ndoa, elimu, kazi, uzoefu na kadhalika. Katika utambulisho ndio unaona capacity (uwezo) wa mtu.

“Kiongozi pia lazima awe na maono. Awe na huruma (akarejea kitabu cha Mathayo 9:35-38, Yesu alipowahurumia makutano). Lazima kuwezesha wasiojiweza, ndiyo maana kuna taasisi za kutoa maji, chakula, elimu, mavazi. (Kiongozi) asipokuwa na macho kwa wahitaji ni tatizo.
“Uongozi ni kutatua matatizo. Pia ni lazima kiongozi ahakikishe kuna uhusiano bora katika taasisi. Kuhakikisha hakuna makundi (ya kimgogoro) kwa watu anaowaongoza. Pa aweke imani katika matendo.”
Awali, Dk Mayala alisema uongozi ni kutoa mchango kutokana na ujuzi, elimu, uzoefu na akili ulizonazo, siyo kutafuta nafasi (positions).
“Uongozi ni uwezo wa kujitoa kwa ajili ya wengine. Kutoa akili, nguvu, maarifa, elimu, uzoefu kwa ajili ya wengine. Nitatoa mfano – kuku, ng’ombe na nguruwe walikutana katika kikao wakajadili watampa nini bwana wao baada ya kuwahudumia kwa uaminifu kwa muda mrefu. Kuku akasema atatoa trei 12 za mayai, ng’ombe akasema atatoa lita 50 za maziwa, nguruwe akasema atatoa soseji. Ni nani aliyejitoa kuliko wote hapo?” alihoja Dk Mayala na wajumbe wakajibu nguruwe kwa kuwa alitoa uhai wake.
Semina hiyo ilihudhuriwa na wajumbe 58 walio na nafasi mbalimbali za kiuongozi.