
MSHAMBULIAJI wa Simba, Moses Phiri, ameweka wazi licha ya ugumu wa michuano ya kimataifa ambayo wanashiriki, bado malengo yake ni kuhakikisha anaifungia timu hiyo mabao ya kutosha ili kuisaidia kufika mbali msimu huu.
Phiri ambaye ni ingizo jipya, tayari amefanikiwa kuifungia Simba bao katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini msimu huu dhidi ya Nyasa Big Bullets wakati Simba ikishinda 0-2.
Akizungumza na Spoti Xtra, Phiri alisema bado anatamani kuendelea kufunga mabao mengi ya kutosha katika michuano hiyo ili kuhakikisha Simba wanafika mbali zaidi na kuzidi kutengeneza historia mpya.
“Bao moja ambalo nimefunga katika michuano ya kimataifa wala sio kwamba kazi imekwisha, hapana, nahitaji kuona nikifunga mabao mengi zaidi katika michuano hii, Simba inahitaji kuvuka pale ilipoishia.
“Hivyo inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia na mimi nahitaji kuwa katika sehemu ya histori hiyo na kubaki katika kumbukumbu za mashabiki wa timu hii ndio maana bado tutaendelea kujituma kwa ajili ya hili ili kukamilisha safari yetu,” alisema Phiri.
Leo Jumapili, Simba inatarajiwa kurudiana na Nyasa Bib Bullets kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, ikiwa na mtaji wa mabao 2-0 ilioupata ugenini.
04 Katika michuano yote msimu huu, Phiri amefunga mabao manne, moja kimataifa na matatu Ligi Kuu Bara.
STORI NA MARCO MZUMBE