
Mashirika mawili yasiyo ya kiserikali Bukoba Developers (BUDES) na Management Development for Health (MDH) yameungasha nguvu ya utoaji elimu juu ya chanjo ya Uvico19 pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko ili kuwezesha wananchi kujitokeza kwa wingi kuchanja.
Mkurugenzi wa BUDES ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Wakili Stephen Byabato(NWN) Wakati akitambulisha shirika la Bukoba Developers(BUDES) amesema shirika hilo limejikita katika sekta ya Elimu, Afya Mazingira, Uchumi na Msaada wa kisheria.
Byabato aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa viongozi wa mitaa na kata kumi na nne, wakiwemo Wenyeviti wa Serikali za mitaa, Watendaji wa kata na mitaa pamoja na Madiwani wa Manispaa ya Bukoba ambapo MDH na BUDES wametao mafunzo kwa viongozi hao kwa lengo la kwenda kutoa elimu na hamasa ya chanjo ya uvico19 Wilaya ya Bukoba Mjini.

Byabato ameongeza kuwa BUDES itatoa vijana kumi na nne watakao tembea nyumba kwa nyumba kata zote kumi nne kwa ajili ya kuhamasisha wananchi juu ya suala la chanjo ya Uvico19 na magonjwa ya Mlipuko.
Akizindua mafunzo hayo ya viongozi wa Manispaa ya Bukoba Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila amesema bado Mkoa wa Kagera mwitikio wa wananchi kuchanja ni mdogo na hivyo viongozi wanao wajibu wa kuendelea kutoa hamasa kwa jamii ili waelewe lengo la serikali kuleta chanjo na umuhimu wake
“Ndugu zangu Serikali inayo nia ya dhati ya kuwakinga wananchi wake dhidi ya ugonjwa wa Uvico19 hivyo haiwezi kuleta chanjo inayodhuru watu wake.”

Kadhalika Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila amekabidhi Pikipiki 76 kwa wahudumu wa afya, zenye thamani ya shilingi milioni Mia mbili na ishirini zilizotolewa na MDH kwa kushirikiana na BUDES ambazo zitasaidia watoa huduma za afya kutoa elimu kwa jamii.