×

Unashangaa Bao 9 Alizopigwa Zalan, Yanga Alishawahi Kumpiga Mtu Bao 14

Jerry Tegete, Mrisho Ngassa pamoja na Simon Msuva enzi wakiwa wachezaji wa Yanga

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, juzi walifanikiwa kutinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Zalan FC ya Sudan Kusini jumla ya mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

 

Yanga inatinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 9-0, kwani wiki moja iliyopita ilishinda mabao 4-0 kwenye uwanja huo huo.

 

Zalan haikucheza mechi yoyote nchini kwao, badala yake iliutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kikanuni kama wa nyumbani Septemba 10 na kupoteza kwa mabao 4-0, kabla ya mechi ya juzi.

Didier Kavumbagu, mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Yanga

Matokeo ya mechi hiyo yameifanya Yanga kutinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa baada ya miaka mitano. Mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2017 ilipoifunga Ngaya Club de Mde ya Comoro kwenye raundi ya awali na kutinga hatua hiyo.

 

Pia, imeweka rekodi ya kutinga hatua hiyo kwa kutoa vichapo vikali kama ambavyo ilivyokuwa ikifanya huko nyuma. Hii si mara ya kwanza kwa timu hiyo kutinga hatua hiyo kwa kishindo ikitoa adhabu kali kwa timu ilizokutana nazo.

 

Katika makala haya tumekukusanyia mechi za raundi ya awali ambazo Yanga ilishinda kwa kishindo, ikitinga raundi ya kwanza, haya sasa…

 

#1. Yanga 7-2 St. Louis (1992)

 

Ni mwaka ambao bado mechi za mabingwa wa Afrika zilikuwa zinatambuliwa kama Klabu Bingwa Afrika. Ilikuwa ni 1992, Yanga ilipoanza raundi ya kwanza kwa kucheza dhidi ya St Louis ya Shelisheli.

Hamis Kiiza Diego, mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Yanga

Kwenye mechi ya kwanza, Yanga ilikwenda ugenini na kuikung’uta timu hiyo mabao 3-1 na mchezo wa marudiano nchini katika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), ilishinda tena kwa mabao 4-1. Matokeo ya jumla yakawa mabao 7-2, Yanga ikatoka kwenye hatua ya awali na kutinga raundi ya kwanza.

 

Hata hivyo, kwenye raundi hiyo ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi Ismailia ya Misri. Kwenye mechi ya kwanza nchini, wageni walishinda mabao 2-1 na Yanga ikaenda kukomaa ugenini nchini Misri na kutoka sare ya bao 1-1, ukawa mwisho wao.

 

#2. Yanga 14-1 Etoile d’Or (2009)

 

Hapa tayari ilianza kuitwa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilicheza dhidi ya Etoile d’Or Mirontsy ya Comoro mwaka 2009. Mechi ya kwanza ilipigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (Sasa Mkapa), Yanga ilipata ushindi wa mabao 8-1.

Fiston Mayele na Aziz Ki

Mkenya Boniface Ambani alipachika mabao manne kwenye mechi hiyo, Jerry Tegete akifunga mawili, Mrisho Ngasa na beki raia wa Malawi Wisdom Ndlovu wakifunga bao moja kila mmoja. Mechi ya marudiano nchini Comoro, Yanga tena ilifanya maangamizi, ikishinda mabao 6-0. Ushindi huo iliifanya kutinga raundi ya kwanza ya ligi hiyo, ambapo ilikutana na Al Ahly ya Misri.

 

Iliishia kwenye raundi hiyo baada ya kuchapwa mabao 3-0 nchini Misri na kukubali kipigo cha bao 1-0 nchini, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0.

 

#3. Yanga 12-2 Komorozine (2014)

 

Yanga ilipata tena karamu ya mabao na kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza kutoka ile ya awali mwaka 2014 ilipocheza dhidi ya Komorozine de Domoni ya Comoro. Iliitoa kwa jumla ya mabao 12-2, ikishinda mabao 7-0 nyumbani na ugenini 5-2.

 

Kwenye mechi ya kwanza, mabao matatu yalifungwa na Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu akifunga mawili, Nadir Haroub Cannavaro na Hamisi Kiiza wakifunga bao moja kila mmoja. Kwenye mechi ya marudiano, yalikuwa tena mabao matatu ya Ngassa ‘hat-trick’, Hamisi Kiiza na Simom Msuva na kuifanya kutinga kwa mara nyingine tena raundi ya kwanza.

 

Kwenye mechi ya raundi ya kwanza, Yanga ilicheza dhidi ya Al Ahly ya Misri, kila timu ikishinda bao 1-0 nyumbani, lakini ikatolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

 

#4. Yanga 6-2 Ngaya (2017)

 

Yanga ilicheza tena Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2017 na kufanikiwa kutinga raundi ya kwanza kwa idadi kubwa ya mabao, safari hii zamu ikiwa ya Ngaya Club de Mde ya Comoro.

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao katika moja ya michezo yake

Kwenye mechi ya kwanza ikichezwa jijini Moroni, Yanga ilishinda mabao 5-1, yaliyofungwa na kiungo Mzambia, Justin Zulu, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko. Mechi ya marudiano, Ngaya ilivimba na kulazimisha sare ya bao 1-1 nchini, Yanga ikasonga mbele raundi ya kwanza kwa ushindi mnono wa mabao 6-2.

 

Ilishindwa kuvuka hatua inayofuata baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa bao la ugenini, ikitoka sare nchini ya bao 1-1,

 

#5. Yanga 9-0 Zalan FC (2022)

Jerry Tegete moja ya washambuliaji hatari waliowahi kupita katika klabu ya Yanga

Miaka mitano imepita, kabla ya Yanga kutinga tena kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoichakaza Zalan FC ya Sudan Kusini mabao 9-0. Hii ni baada ya msimu uliopita kutolewa dhidi ya Rivers United kwenye hatua za awali za michuano hiyo, ilipofungwa jumla ya mabao 2-0, bao 1-0 kila mechi.

 

Straika Fiston Mayele alifunga mabao sita kwenye idadi hiyo, kila mechi akipiga ‘hat-trick’. Kwenye mechi ya kwanza alifunga mabao matatu, moja likifungwa na Feisal Salum, na mechi ya marudiano Mayele alifunga tena matatu, Stephane Aziz Ki akifunga bao moja na Farid Mussa.

Leave a Comment