×

Kocha wa Yanga Atumia Dakika 90 Kuwamaliza Al Hilal Ligi ya Mabingwa

Wachezaji wa timu ya Yanga.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Mrundi, Cedric Kaze, juzi walijifungia ndani kwa dakika 90 na kuungalia mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Hilal dhidi ya St George.

 

Katika mchezo huo uliochezwa nchini Sudan, Al Hilal wakiwa wenyeji walishinda bao 1-0 na kufanikiwa kufuzu hatua ya kwanza ya michuano hiyo ambapo sasa watakwenda kupambana na Yanga kuwania kutinga hatua ya makundi.

 

Yanga ilikuwa ya kwanza kutinga hatua ya kwanza baada ya kuiondosha Zalan FC kwa jumla ya mabao 9-0, huku mshambuliaji wake, Mkongomani, Fiston Mayele akipiga hat trick mbili katika michezo miwili.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi.

Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema akiwa na Kaze, waliufuatilia mchezo huo kwa ukaribu na kikubwa kufahamu mbinu, udhaifu wao na wachezaji hatari wa kuchungwa.

 

Nabi alisema ameona ubora wa Al Hilal ambao ameuficha kwa kukataa kuuweka wazi kwa kuhofia wapinzani kushtuka, zaidi akipanga kukiimarisha zaidi kikosi chake ili kuhakikisha anapata ushindi nyumbani na ugenini.

 

“Mimi ni kama mwanajeshi, muda wowote nipo tayari kwa ajili ya mapambano, hivyo kukutana na Al Hilal nilitarajia.

 

“Hivyo kama kocha nimekuwa na utaratibu wa kuwafuatilia wapinzani wangu kwa kuziangalia video za michezo yao ya mwisho waliyocheza kwa ajili ya kuwajua zaidi.

 

“Wapinzani wetu Al Hilal tayari nimewaona na kuwafahamu wachezaji hatari wa kuchungwa, mbinu na mfumo wanaoutumia, kikubwa ninaendelea kukinoa kikosi changu kitakachopata ushindi,” alisema Nabi.

 

Yanga itaanzia nyumbani dhidi ya Al Hilal ambapo mechi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa kati ya Oktoba 7 na 9, kisha marudiano ni Sudan kati ya Oktoba 14 na 16, mwaka huu.

Leave a Comment