
TAARIFA zimeibuka juu ya usajili wa kimya kimya wa mshambuliaji wa klabu ya RB Leipzig ya nchini Ujerumani raia wa Ufaransa Christopher Nkunku kujiunga na klabu ya Chelsea mapema msimu ujao majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Bild la nchini humo, Christopher Nkunku alifanya vipimo vya afya chini ya usimamizi wa madakari wa Chelsea katika jiji la Frankfurt ikiwa ni hatua ya makubaliano ya kujiunga na Chelsea msimu ujao.

Taarifa zimebainisha kuwa zoezi hilo lilifanywa kwa siri huku kukiwa na makubaliano ya klabu ya Chelsea kulipa kiasi cha Euro milioni 60 kama sehemu ya malipo ya kuvunja mkataba alionao kwa sasa na RB Leipzig.
Klabu ya Chelsea imekuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na timu za Ujerumani hasa ikiwemo RB Leipzig ambayo pia kwa misimu miwili iliyopita ilikubali kuwauzia mshambuliaji raia wa Ujerumani Timo Werner ambaye msimu huu amerejea ndani ya viunga vya klabu hiyo baada ya mambo yake kutomwendea vyema katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Mapema majira ya kiangazi msimu huu Christopher Nkunku aliongeza mkataba mpya wa miaka miwili ambao unatarajia kumuweka ndani ya klabu hiyo hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2026, kama Chelsea itafanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji huyo basi itakuwa imepata boja kati ya washambuliaji hatari zaidi duniani kwa upande wa vijana katika soka kwa sasa.