
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amempigia simu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuagiza kuwa kijana aliyesaidia kuokoa watu waliokuwa wamekwama ndani ya ndege baada ya kutokea ajali ya Precision Air, aingizwe kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kijana huyo, Majaliwa Jackson, ameonesha ushujaa wa hali ya juu kwa kufanikiwa kufungua mlango wa ndege na kuwaokoa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Aidha katika kutambua mchango wake wadau wengine wamempongeza kijana huyo kwa kumpatia pesa taslimu ikiwemo kiasi cha shilingi milioni moja kilichotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila, Kiasi cha Shilingi milioni mbili kilichotolewa na Shirika la Ndege la Precision Air pamoja na baadhi ya taasisi nyingine binafsi.